Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Rais Samia Awatunuku Kamisheni Maafisa Wanafunzi 740

Wananchi Wafurika Banda la Ofisi ya Waziri Mkuu Kupata Elimu

Na Mwandishi Wetu – MWANZA

Wakazi wa mkoani Mwanza na maeneo ya jirani ya mkoa huo wamejitokeza kwa wingi kupata elimu ya Sekta ya Hifadhi ya Jamii kwenye banda la Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi Vijana Ajira na Watu Wenye Ulemavu ambapo kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii na Mifuko ya PSSSF, NSSF na WCF. 

Hayo yamejiri katika maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha yanayoendelea katika viwanja vya Rock City Mall, jijini humo yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Elimu ya Fedha kwa Maendeleo ya Watu.”

 Akizungumza na wananchi waliotembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Hifadhi ya Jamii, Bw. Omary Mziya ameeleza kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kupitia Idara ya Hifadhi ya Jamii ina wajibu wa kusimamia, kuratibu na kujenga mazingira wezeshi yanayolenga kuendeleza sekta ya hifadhi ya jamii nchini. 

Makamu wa Rais Afanya Ziara ya Siku Moja Ukerewe

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango leo tarehe 25 Novemba, 2022 amefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza.

Akiwa ziarani visiwani humo, Makamu wa Rais amefungua rasmi shule ya sekondari ya Ukerewe iliyopo kata ya Kagunguri iliyogharimu Shilingi bilioni 1.1 katika ujenzi wake.

Makamu wa Rais ameiagiza TAMISEMI kuhakikisha shule hiyo inawekewa miundombinu ya somo la fizikia ikiwemo maabara ya somo hilo ili iweze kukamilisha dhana ya sayansi. Pia Makamu wa Rais ameagiza ujenzi wa shule kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwemo kuweka miundombinu rafiki kwa masomo ya TEHAMA.

Akiwa shuleni hapo Makamu wa Rais amewasihi wazazi na walezi kusimamia watoto wao wapate elimu ili wawe msaada sahihi kwa maendeleo ya taifa. Amesema tatizo la mimba za utotoni limekua kubwa wilaya ya Ukerewe na hivyo kurudisha nyuma jitihada za Serikali katika kuboresha elimu wilayani hapo.

Makamu wa Rais amesema Serikali inaendelea na jitihada za kujenga miundombinu bora ya elimu pamoja na kutoa elimu bila malipo kwa elimu ya msingi na sekondari ili kuhakikisha taifa linapata wataalamu wenye tija.

Wito Watolewa kwa Vyuo Nchini Kuhakikisha Elimu Inaendana na Mabadiliko ya Teknolojia

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa vyuo vyote hapa nchini kuhakikisha elimu inayotolewa inaendana na mabadiliko ya teknolojia yanayoendelea kwa kasi duniani na vipaumbele vya kitaifa ikiwemo ujenzi wa uchumi wa viwanda na uchumi wa buluu.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2022 akiwa Mgeni Rasmi katika Mahafali ya 41 ya Chuo Huria Tanzania yaliofanyika katika Uwanja wa Furahisha Jijini Mwanza. Amesema ni lazima kujipanga kutoa elimu iliyo bora na hasa inayolenga kuwajengea wahitimu uwezo wa kujiajiri na zaidi kuwa na ubunifu ambao utawasaidia kushiriki katika fursa zinazojitokeza na kujenga mihimili ya Taifa kiuchumi na kiteknolojia.

Makamu wa Rais amesema ili Tanzania iweze kuwa nchi ya uchumi wa kati inayoongozwa na viwanda ni lazima kuwa na mifumo bora ya elimu hususan elimu ya juu. Ameongeza kwamba Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya elimu ya juu na ufundi stadi kwa kuimarisha miundombinu, kuongeza bajeti kwenye sekta hiyo kila mwaka na kuendelea kuboresha sera ya elimu hapa nchini. Pia ametoa rai kwa wanazuoni wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na vyuo vingine vyote hapa nchini, kutumia weledi na utaalamu wao katika zoezi la maboresho ya elimu.

Pia, amewasihi wahitimu wa Chuo hicho kudhihirisha elimu waliopata katika utendaji wa kazi na maisha ya kila siku, iwe ni katika sekta rasmi au sekta isiyokuwa rasmi. Amesema ni lazima kuonesha utofauti katika kutafuta majibu ya maswali mbalimbali yanayowakabili Watanzania katika jitihada zao za kujiletea maendeleo.

Makamu wa Rais amesema kwamba Serikali imejipanga kuona sekta ya elimu inaboreshwa zaidi ili kukidhi mahitaji na kuweza kuendana na jitihada za kuleta maendeleo endelevu nchini ikiwemo kuendelea kuboresha mazingira ya Vyuo na kuongeza idadi katika mikoa yetu yote ili wananchi zaidi wapate fursa ya kujiendeleza kimasomo na kupata elimu ya juu.

Rais Samia Awataka EALS Kutenda Haki

Na Daudi Manongi, ARUSHA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wanasheria kusimamia haki katika kesi mbalimbali wanazozisimamia.

Mhe. Rais Samia amesema hayo leo tarehe 24 Novemba, 2022 wakati akifungua mkutano wa 27 wa Jumuiya ya Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) uliofanyika katika hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

“Msipofanya haki, mnapomtia mtu hatiani
kwa rushwa ambaye hana hatia na mwenye hatia mkamuachia anatembea huru yule mwenye hatia anakwenda kuendeleza ubabe na kuvunja sheria akijua pesa yake itambeba na yule ambaye hana pesa anaishia jela”, amesema Rais Samia.

Aidha, ametoa rai kwa Jumuiya hiyo kuendelea kushirikiana bega kwa bega na vyama vingine vya Wanasheria wa kitaifa ili kukuza utoaji wa haki na kusimamia uzingatiaji wa sheria katika Jumuiya yetu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Geophrey Pinda ametoa rai kwa wanasheria nchini kujiunga na Jumuiya ya Wanasheria Afrika Mashariki kwa sababu ni chombo muhimu kitakachowatangaza ndani na nje ya nchi.

Majaliwa Atembelea Soko Kuu la Wafanyabiashara Wadogo Jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi mbalimbali wakati alipowasili kwenye Soko la Wafanyabiashara wadogo lililopo Bahi Road jijini Dodoma kukagua soko hilo na kuzungumza na wafanyabiara hao, Novemba 24, 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua eneo la kuuzia mboga, viungo na matunda katika Soko Kuu la Wafanyabiashara Wadogo lililopo Bahi Road jijini Dodoma, Novemba 24, 2022

Majaliwa Akagua Ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa – SGR Jijini Dodoma

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR)  ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma, Novemba 24, 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa  (kulia) wakati alipokagua ujenzi wa Stesheni Kuu ya Reli ya Kisasa (SGR)  ya Dodoma katika eneo la Mkonze jijini Dodoma, Novemba 24, 2022. Wa nne kulia ni Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. Festo Dugange.
ev eşyası depolama