Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha vijana wanapata fursa zaidi za kiuchumi kupitia Sekta ya Madini, ambayo imeendelea kuwa moja ya sekta muhimu katika kukuza uchumi wa nchi na kuchagiza maendeleo ya sekta nyingine.
Kupitia Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya mwaka 2025, Serikali imeweka vipaumbele maalum vinavyolenga kuwawezesha vijana katika ajira, kukuza ujuzi wa kisayansi pamoja na kuimarisha uwekezaji katika sekta ya madini nchini.
Hayo yameelezwa leo Machi 16,2026 Jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari.
“ Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa madini, kuwapatia leseni pamoja na kuwaendeleza ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchimbaji na biashara ya madini. Hatua hii inalenga kuongeza ushiriki wa vijana katika uchumi wa madini na kuwapa fursa ya kujiajiri na kuajiri wengine,” amesema Mhandisi Kamando.

Ameongeza kuwa Serikali imejipanga kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu cha biashara ya madini katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa kuimarisha masoko ya madini na vito.
Ambapo jengo la Tanzanite Exchange Centre (TEC) linajengwa katika eneo la Mirerani, Wilaya ya Simanjiro, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza thamani ya madini ya Tanzanite na kutoa fursa zaidi za biashara kwa vijana.
Aidha, amesema katika kuongeza manufaa ya madini kwa taifa, Serikali pia inaendelea kuhamasisha na kusimamia shughuli za uongezaji thamani wa madini ndani ya nchi. Mkakati huo unalenga kuhakikisha madini yanachakatwa na kuongezewa thamani kabla ya kuuzwa nje ya nchi, jambo litakalosaidia kuongeza ajira na kukuza ujuzi kwa vijana.

Mhandisi Kamando ameendelea kufafanua kuwa kutokana na umuhimu wa madini adimu na ya kimkakati katika uchumi wa dunia, Serikali imeweka mazingira maalum ya kisera na kisheria yatakayohakikisha uchimbaji wa madini hayo unafanyika kwa ubia kati ya Serikali na wawekezaji kutoka nje.
Sambamba na hilo, sera, sheria na kanuni zinaandaliwa ili kuhakikisha madini hayo hayasafirishwi nje ya nchi bila kuongezewa thamani hapa nchini.
Pia, amesema hatua hizo zinaonesha dhamira ya Serikali ya kutumia rasilimali madini kama chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku vijana wakipewa nafasi kubwa ya kushiriki na kunufaika na fursa zinazotokana na sekta hiyo muhimu.