Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini kwa mwaka wa fedha 2025/2026 imetenga bajeti ya jumla ya shilingi 25,335,000,000 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo Machi 2026, katika ukumbi wa Idara ya Habari - MAELEZO Mtumba, jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Hamisi Kamando wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu miradi ya maendeleo na fursa kwa vijana.
Mhandisi Kamando amesema ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo, Tume inatekeleza jukumu la kuimarisha usimamizi wa Sekta ya Madini na ukusanyaji wa mapato ya Serikali yatokanayo na rasilimali madini pamoja na kuvutia uwekezaji ikiwemo kuboresha mazingira ya upatikanaji madini.
Aidha, amesema fedha hizo zinatumika katika ununuzi wa vitendea kazi mbalimbali kama vile magari, mashine za utambuzi wa madini ya metali (XRF) zitakazotumiwa na watalaam katika kutoa huduma kwa wananchi katika masoko ya madini na baadhi ya migodi mikubwa ya kati na midogo.

"Pamoja na mambo mengine katika kuboresha huduma bora kwa wananchi, Tume inagharamia mafunzo maalum ya kitaalam kwa watumishi ili kuwaongezea ujuzi katika kutoa huduma kwa wananchi,” amesema Mhandisi Kamando.
Ameongeza kuwa, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeendelea kutenga maeneo ya uchimbaji wa madini kwa ajili ya wachimbaji wafogo wa madini nchini ili kwa pamoja waweze kufaidika na rasilimali zilizopo nchini.
Amesisitiza “Maeneo yanayotengwa na kugawiwa kwa wananchi sehemu kubwa yanawalenga vijana kati ya umri wa miaka 18 hadi 45. Hadi sasa jumla ya maeneo 65 yamependekezwa kutengwa kwa ajili ya kugawiwa kwa wachimbaji wadogo katika mikoa ya kimadini ya Mtwara, Manyara, Lindi, Morogoro, Dodoma, Tabora, Pwani, Tanga, Geita, Shinyanga, Mwanza, Mara, Mbeya na Ruvuma.”
Pamoja na hayo, amesema kuwa kufikia Desemba 2025, Tume ya Madini imewezesha vijana 2,550 kupata ajira za moja kwa moja kupitia Mradi wa Mageuzi katika Sekta ya Madini kwa Maendeleo Jumuishi na Endelevu (MBT).