Naibu msajili wa vyama vya siasa Mh. Mohamed Ahmed Ally amesema kuwa uelewa wa sheria ya gharama za uchaguzi umeongezeka kwa vyama vya siasa nchini katika chaguzi zilizofanyika hivi karibuni tofauti na zilizopita.
Mh.Ally ameyasema hayo leo Machi 10, 2026 katika warsha ya marejesho ya gharama za uchaguzi kwa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu wa 2025 , iliyofanyika kwenye ukumbi wa Karimjee Jijini Dar- es- salaam.

Amesema kuwa hapo mwanzo vyama vingi vya siasa nchini vilikuwa havijazi fomu ya mrejesho wa gharama ya uchaguzi kama ilivyoorodheshwa kwenye kanuni za uchaguzi ,12(1) ambayo inavitaka vyama vya siasa kuweka bayana gharama zilizotumika katika kipindi chote cha kampeni na uchaguzi, na kuifanya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kuchukua hatua ya kutoa elimu juu ya umuhimu wa vyama hivyo kuweka bayana taarifa hizo .
Amesema kuwa kufanyika warsha mbalimbali za elimu juu ya gharama za uchaguzi kumeongeza hamasa kwa vyama vya siasa kutoa mrejesho wa gharama walizotumia wakati wa uchaguzi kufikia asilimia sabini (70%) mpaka sasa.

Aidha Mh.Ally ameongeza kuwa sheria ya gharama za uchaguzi ina lengo la kuweka uwanja sawa kwa vyama siasa kati ya mwenye nacho na asiye kuwa nacho.
" Tumeitana hapa leo tukiwa na lengo mahususi la kuendelea kuelewashana namna ya kujaza fomu za gharama za uchaguzi na kuendelea kukumbushana juu ya umuhimu wa sheria ya gharama za uchaguzi", Amesema Mh. Ally.

Naye aliyekuwa mgombea kiti cha Uraisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupita chama cha NLD Mh.Doyo Hassan Doyo ameipongeza serikari kupitia kwa msajili wa vyama vya siasa kwa kuandaa warsha hiyo ambayo itawapa uwanda mpana wadau wasiasa kwa kuwa na uelewa wa pamoja juu ya sheria ya gharama za uchaguzi na kuvifanya vyama vyote vya siasa vishiriki uchaguzi kwa kuzingatia usawa na haki yakutokuwa na matumizi mabaya ya fedha katika kipindi cha uchaguzi.
Kwa mujibu wa kanuni za gharama za uchaguzi 12(1), imeweka ukomo wa gharama za kampeni za vyama vya siasa ,ambapo ukomo wa vyama vya siasa ni tsh, bilioni 17, urais bilioni 6, na udiwani ni milioni 8.