Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Yaridhishwa na Utoaji wa Huduma za Kibingwa Bobezi Muhimbili
Mar 16, 2026
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI Yaridhishwa na Utoaji wa Huduma za Kibingwa Bobezi Muhimbili
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI wakioneshwa maeneo mbalimbali ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) wakati walipofanya ziara yao katika Hospitali hiyo leo tarehe 16 Machi 2026
Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, leo tarehe 16 Machi 2026 imefanya ziara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa lengo la kukagua utoaji wa huduma za afya pamoja na kujionea utekelezaji wa miradi na maboresho mbalimbali yaliyofanyika katika hospitali hiyo.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Dkt. Johannes Lukumay amesema kamati imeridhishwa na maendeleo ya utoaji wa huduma pamoja na juhudi zinazofanywa na uongozi na watumishi wa MNH katika kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi.

“Tumeshuhudia maboresho makubwa ya miundombinu na huduma za afya hapa Muhimbili, haya ni matokeo ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha sekta ya afya, jambo linalochangia kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi,” amesema Mhe. Dkt. lukumay.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati wametembelea baadhi ya vitengo vya hospitali ikiwemo Idara ya Magonjwa ya Dharura na Ajali, Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD), Idara ya Radiolojia, Huduma ya Tiba Hewa Mgandamizo, VIP Kliniki, Jengo la Wazazi linaloendelea kukarabatiwa pamoja na Jengo la IPPM.

Hii ni sehemu ya utaratibu wa Kamati ya Kudumu ya Bunge kufanya ukaguzi wa miradi na huduma za afya nchini, ikiwa na lengo la kujiridhisha na utekelezaji pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali kuhusu maeneo yanayohitaji kuboreshwa.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi