Karibuni kwenye Blogu Rasmi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Huu ni Uwanja wa Wananchi Kupata Taarifa Mbalimbali za Serikali na Masuala Mengine ya Kijamii, Kisiasa, na Kiuchumi. Blogu hii inaratibiwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kupitia Idara ya Habari (MAELEZO).

Waziri Hasunga Awapongeza Wanunuzi wa Pamba Shinyanga wa Kuwalipa Wakulima kwa Wakati

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Shinyanga.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga leo Agosti 10, 2020 amefanya ziara ya kikazi mkoani Shinyanga ambapo amekagua na kuridhishwa na hali ya ununuzi wa msimu wa pamba kwa mwaka 2020/2021.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha kuchambua Pamba cha Afrisian, Aham, GAKI na Fresho, Waziri Hasunga amewapongeza wamiliki wa kampuni hizo kwa mapokezi mazuri ya pamba pamoja na kuwalipa wakulima kwa wakati.

HESLB Walivyofafanua Hoja na Maswali ya Waombaji Mikopo wa Elimu ya Juu Mikoa ya Kigoma na Geita

Afisa Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Winfrida Wumbe akizungumza na wanafunzi wa Shule za Sekondari za Kalangalala na Shule ya Sekondari na wa wahitimu wa masomo ya kidato cha sita wakati wa kampeni ya utoaji elimu kuhusu mwongozo wa utoaji mikopo kwa wanafunzi ea Elimu ya Juu kwa mwaka 2020/2021. Mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Geita Mkoani Geita tarehe Julai 27, 2020

Na Ismail Ngayonga

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) hivi karibuni imefungua dirisha la maombi ya mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na masomo ya Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa  masomo 2020/2021.

Kufunguliwa kwa dirisha hilo kunatoa fursa kwa Wanafunzi mbalimbali waliohitimu masomo ya kidato cha sita na ngazi ya stashahada kutoka katika vyuo mbalimbali nchini kutuma maombi ya mikopo ya elimu ya juu ili kuwezeshwa na serikali katika gharama za ada, chakula na malazi pindi wawapo masomoni.

Daraja la Mkapa, Mto Rufiji Mkoani Pwani

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akipita na kukagua Daraja la Mkapa linalopita katika Mto Rufiji mkoani Pwani wakati akitokea Masasi Mtwara kwenye msiba wa Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa leo tarehe 30 Julai 2020. Daraja hilo linalounganisha Pwani na Mikoa ya Lindi na Mtwara lilijengwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Marehemu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Benjamin William Mkapa

TBS Yatoa Elimu Madhara ya Sumukuvu

Na Neema Mtemvu – TBS

Wananchi  wa Handeni wakipata elimu wakipata kuhusiana na sumukuvu

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa elimu kuhusiana na sumukuvu, madhara yake na jinsi ya kukabiliana na tatizo hilo ili kujenga uelewa kwa wananchi wa Wilaya za Handeni na Kilindi mkoani Tanga.

Akizungumza hivi karibuni wakati wa utoaji elimu hiyo, Afisa Usalama wa Chakula Mkuu wa TBS, Dkt. Candida Shirima alisema elimu hiyo imetolewa kwenye wilaya hizo kwa kuwa zipo kwenye ukanda wenye hali ya hewa inayowezesha ustawi wa fangasi wanaozalisha sumukuvu kwenye mazao ya chakula.

“TBS imekuwa ikitekeleza mikakati mbalimbali ili kukabiliana na tatizo la sumukuvu kwa lengo la kulinda afya ya jamii na kuwezesha biashara ya mazao ya chakula”, alisema Dkt. Shirima.

Ratiba ya Mazishi ya Mzee Mkapa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa ataagwa Kitaifa Jumanne Julai 28 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam na atazikwa kijijini kwao Lupaso, Masasi mkoani Mtwara Jumatano, Julai 29, 2020.

“Mwili wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu utaanza kuagwa kuanzia Jumapili, Julai 26, 2020 katika Uwanja wa Uhuru ambapo saa 4.00 asubuhi kanisa Katoliki litaongoza ibada na baada ya ibada waombolezaji wataanza kuaga.”

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Ijumaa, Julai 24, 2020) wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye Makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam. Ametumia fursa hiyo kuwasihi wanafamilia na Watanzania waendelee kumuombea marehemu kwa Mwenyezi Mungu kwa sababu yote ni mapenzi yake.

Serikali Yaomboleza Kifo cha Rais Mstaafu, Mhe. Benjamin Mkapa

Yawasihi wanafamilia na Watanzania waendelee kuwa watulivu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametia saini kitabu cha maombolezo ya kifo cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin William Mkapa kilichotokea jijini Dar es Salaam na ametoa pole kwa familia kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Serikali.

“Ndugu wanafamilia, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali tumepokea taarifa za msiba wa mzee wetu, kiongozi wetu Rais wa Awamu ya Tatu kwa masikitiko makubwa. Nawasihi muendelee kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki kigumu kama alivyosema Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Magufuli.”

Katibu Mkuu Katiba na Sheria Awataka Polisi, Magereza Kuhakikisha Haki za Mtoto Zinalindwa

Na. Karimu Meshack, Mbeya

Serikali imewataka Polisi na Magereza nchini kuhakikisha haki na maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria zinalindwa na kuhifadhiwa kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya 2009.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome wakati akifungua mafunzo ya siku nne kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi na Magereza kutoka katika Mikoa ya Iringa na Mbeya kuhusu utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria kwa watoto jana katika ukumbi wa Mahakama ya Tanzania Kanda ya Mbeya- jijini Mbeya.

Prof. Mchome amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau wakiwemo UNICEF na wengine, imeendelea kuzingatia maslahi ya mtoto anayekinzana na sheria kwa kuhakikisha kuwa shauri linalomhusu linapewa kipaumbele na linashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto.

Rais Magufuli Awaapisha viongozi Aliowateua Hivi Karibuni

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 20 Julai, 2020 amewaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni, Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma.

Hafla ya kuapishwa kwa viongozi hao imehudhuriwa na Makamu wa Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Wakuu wa Mikoa, Makatibu Wakuu na viongozi wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama.

Mhe. Rais Magufuli amewaapisha Mhandisi Marwa Mwita Rubirya kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dkt. Aloyce Kashindye Nzuki kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Anthony Damian Sanga kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Dkt. Sief Abdallah Shekalaghe kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Allan Herbert Kijazi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhandisi Nadhifa Sadiki Kemikimba kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt. Mwinyi Talib Haji kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.