Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Jafo Aongoza Mapokezi ya Treni ya Mwendokasi Dodoma
Apr 21, 2024
Waziri Jafo Aongoza Mapokezi ya Treni ya Mwendokasi Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akiongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika mapokezi ya treni ya mwendokasi ya majaribio iliyobeba viongozi wa dini waliosafiri kwa treni ya mwendokasi wakitokea Dar es Salaam leo Aprili 21, 2024.
Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewaongoza viongozi na wananchi wa Mkoa wa Dodoma katika mapokezi ya viongozi wa dini waliosafiri kwa treni ya mwendokasi wakitokea Dar es Salaam leo Aprili 21, 2024.

 

Viongozi hao wanatarajia kushiriki ibada maalumu ya kuliombea Taifa itakayofanyika katika Uwanja wa Jamhuri Aprili 22, 2024 na kuongozwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango.

 

Akizungumza mara baada ya treni hiyo kuwasili, Dkt. Jafo amesema hiyo ni fahari kubwa kwa nchi yetu kupata usafiri huo ambao pamoja ya kwamba unatumia muda mfupi kusafiri lakini pia umewaunganisha Watanzania wote kwani kuna wengine wametoka Pemba na Unguja.

 

Amesema wakati Taifa linaelekea kuadhimisha miaka 60 ya muungano hayo ni mafanikio makubwa katika sekta ya usafiri kwani kupitia muungano, wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar wanajenga uchumi kwa mafanikio makubwa ya nchi.

 

Dkt. Jafo ameongeza kuwa kwa vile serikali imefanya uwekezaji mkubwa wa reli ya kisasa, imeona ni jambo la heri viongozi wa dini wawe wa kwanza kupanda chombo hicho wakati wanakwenda kuliombea Taifa.

 

Amesema Tanzania ni Taifa la mfano duniani ambalo wananchi wake kutoka Bara na Zanzibar wameungana na kujenga uhusiano wa damu ambao umedumu kwa kipindi kirefu. 

 

“Ndugu zangu najua mmetoka mbali tunawakaribisha sana Dodoma, lakini naomba niwaambie viongozi wa dini kuwa serikali inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda sana na kesho tutakuwa na maombi ya kuliombea Taifa letu kwa tunu ya muungano tuliyonayo,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wakati wa mapokezi ya treni ya mwendokasi iliyobeba viongoza wa dini waliowasili mkoani Dodoma wakitokea Dar es Salaam leo Aprili 21, 2024. 

Akielezea namna maadhimisho hayo yatakavyoadhimishwa, Dkt. Jafo amesema kuwa serikali imeamua kufanya maombi maalumu tarehe 22 na tarehe 24 kutakuwa na tuzo maalumu kwa waasisi wa muungano, tarehe 25 kutakuwa shamrashamra za muungano jijini Dar es Salaam na kufuatiwa na kielele cha maadhimisho hayo Aprili 26, 2024.

 

Miongoni mwa waliosafiri na treni hiyo kutoka jijini Dar es Salaam ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Cyprian Luhemeja pamoja na watendaji kutoka ofisi ya Makamu wa Rais.

 

Viongozi walioshiriki katika mapokezi hayo ni Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi