Na Jacquiline Mrisho.
Wananchi wa Kijiji cha Melela kilichopo wilayani Mvomero mkoani Morogoro wamekiri kuwa uelewa wao kuhusiana na masuala ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi umeongezeka baada ya kupata mafunzo yanayoendeshwa na Shirika la PELUM Tanzania.
Hayo yamebainishwa hivi karibuni mkoani Morogoro na Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Mvomero, Basil Makunza wakati akihitimisha mafunzo hayo yaliyofanywa kwa viongozi wa Baraza la Ardhi la Kijiji, Kamati ya Maamuzi, Wajumbe wa Serikali ya Kijiji, Wakulima wawezeshaji na wananchi wa kawaida.
Makunza alisema mafunzo hayo yamewasaidia wanakijiji kuwa na uelewa mkubwa juu ya mpango wa matumizi ya ardhi hali iliyopelekea kupunguza na kuondoa migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiendelea kwenye Vijiji vya mradi.
“Kwa sasa wananchi wa kijiji chetu wana uelewa mkubwa juu ya mipango ya ardhi lakini nawasisitiza pia kufuata Sheria ndogondogo walizojipangia ikiwemo kuwepo kwa ushirikiano madhubuti kati ya ngazi ya kijiji na wataalamu wa Wilaya ya Mvomero,”alisema Makunza.
Makunza aliongeza kuwa, mbali na kupata elimu kaya mbalimbali zimebadili fikra za maisha ikiwemo wanaume kukubali kuruhusu wenza wao kumiliki ardhi waliyoitafuta pamoja na hata kufikia hatua kukubali kuweka picha mbili ya mke na mume kwenye hatimiliki ili kuonyesha umiliki wa pamoja kama njia mojawapo ya kuzuia mtafaruku pindi mmoja wapo atakapofariki ama wakitaka kugawana mali kama watatengana.
Kupitia zoezi hilo la kukamilisha Mpango wa matumizi ya Ardhi kwa kijiji cha Melela, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Amini Membe amesema kwa sasa wanaendelea na michakato wakishirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero kuhakikisha masijala ya ardhi ya Kijiji inakamilika ili wakati watakapopata hatimiliki wazihifadhi kwenye masijala hiyo kuliko kukaa nazo nyumbani.
“Kupitia mafunzo haya, wataalamu kupitia timu iliyoundwa na kupewa mafunzo na PELUM wamekubaliana na wananchi wote kutekelezwa kwa mpango wa matumizi ya ardhi kwa kuandaa ramani ya Kijiji na kumega baadhi ya maeneo ya akiba ili wawape Vijana kwa ajili ya kupata maeneo ya kazi,” alisema Membe.
Nae mmoja wa wakulima wawezeshaji, Bahati Mwinjimvua amesema kuwa kwa upande wake anaendelea na kazi ya kuelimisha wananchi wenzake hasa wanawake umuhimu wa maeneo yao kupimwa na kufikia hatua ya kupata hatimiliki ya ardhi zao.
“Kupitia mafunzo haya yanayotolewa na shirika la PELUM Tanzania nimejua Mwanamke ninapaswa kumiliki ardhi kisheria na kupata hatimiliki yenye jina langu jambo ambalo linasaidia hata mwenzangu atakapoitwa mbele za haki nisidhulumiwe ardhi yangu na ndugu wa mume ama kuuzwa kinyemela na mtu yeyote,” alisema Bi. Bahati.
Naye Mkulima Luisa Lugata amesema hakujua moja ya sababu ya kuongezeka kwa migogoro ya ardhi ni kuongezeka kwa watu pasipo ardhi kuongezeka na hivyo kuchangia watu kukosa maeneo ya makazi, malisho na Kilimo hivyo kuanza kugombania ardhi finyu iliyopo.
Mkazi wa Mvomero Ramadhani Omari alisema, hakujua kuwa si sahihi kutumia,kuuza,ama kugawa ardhi kiholela bila kushirikisha Mamlaka husika ingawa ardhi hiyo ameirithi kutoka kwa Wazazi wake.
“Kwa sasa nafahamu kuwa suala la umiliki wa ardhi lipo kisheria na linasisitiza juu ya hatimiliki pia nimetambua kuwa mtu akitaka ardhi ni muhimu kuomba kwenye Serikali ya Kijiji mbele ya wanakijiji kupitia mkutano Mkuu wa kijiji ili waridhie muhusika kupewa ardhi hiyo”, alisema Omari.
PELUM Tanzania inatekeleza Mradi wa Ushiriki wa Wananchi katika Kusimamaia Sekta ya Kilimo. Tangu mwaka 2013 hadi 2017, jumla ya Vijiji 30 kutoka Wilaya za Kilolo, Mufindi, Morogoro, Mvomero, Kongwa na Bahi, vimenufaika na mradi huo.