Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza fedha zilizotakiwa kutumika kwa ajili ya kugharamia sherehe za maadhimisho ya Uhuru Desemba 9, 2025, zitumike kukarabati miundombinu iliyoharibiwa kwenye vurugu za Oktoba 29.
Hayo yamesemwa leo Novemba 24, 2025 Jijini Dar es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akizungumza na wakazi wa Dar es Salaam katika eneo la Mbezi Luis, mara baada ya kukagua miundombinu iliyoharibiwa kwenye vurugu hizo.
"Tarehe Tisa Disemba mwaka huu, hakutakuwa na sherehe, na gharama za fedha zilizokuwa zitumike kwenye sherehe zitakwenda kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa, kwa hiyo sekta zinazohusika, ratibuni hilo ili fedha hizo ziende haraka, ziende kuponya maisha ya Watanzania, niwaombe twendeni sote kwa kauli moja, tushauriane kuanzia ngazi ya familia, tukubaliane mambo haya yasitokee tena, kama kuna tofauti zetu tukae tukubaliane, tukae tujenge, Rais ameonesha utayari wa hali ya juu kabisa, milango ipo wazi, tumeona madhara yake, mengine hayalipiki, tuiache kabisa njia hiyo twendeni tukae, mambo mengine yanayohusu nchi tutayasimamia ili Tanzania irejee kwenye heshima yake", amesema Dkt. mwigulu
Amesema Tanzania ni mali ya Watanzania na kuwataka kudumisha amani na mshikanano huku akiwataka vijana kuitumia Wizara mpya ya Vijana katika kuijenga nchi.
"Tanzania ni mali ya Watanzania, amani ya Tanzania haina mbadala, tulinde nchi yetu kwa namna yoyote ile, vijana nawaomba mtumie wizara yenu hii katika kuangalia changamoto zinazowakabili, Rais ameunda Wizara hii mahsusi kwa ajili yenu", amesema Dkt. Mwigulu
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba, leo November 24, 2025, amekagua miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (DART) pamoja na mali nyingine zilizoharibiwa kutokana na vurugu zilizojitokeza Oktoba 29, 2025 siku ya Uchaguzi Mkuu.