Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa wito kwa wananchi hususani vijana kuepuka uchochezi unaofanywa na watu wanaoishi nje ya nchi, ambao hawaguswi na madhara ya matendo wanayohamasisha vijana hao wafanye ndani ya Tanzania kwa kisingizio cha kudai haki.
-
Msigwa ametoa wito huo leo Novemba 23, 2025 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuelezea madhara ya vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani vilivyotokea Siku ya Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ambavyo vimewaumiza Watanzania wenyewe huku wachochezi wakiwa salama katika nchi nyingine, wakila na kuishi bila wasiwasi.
“Nawasihi Watanzania kujiepusha kushabikia na kusambaza taarifa ama habari zinazochochea hasira na kuvunja umoja wetu wa Kitaifa.tukiendekeza uchochezi unaofanywa na watu ambao wapo nje ya nchi na hawaguswi na chochote juu ya maisha yetu, tutakaoumia ni sisi ”, amesema Msigwa
Aidha, amewaomba Watanzania waendelee kuwa watulivu na waepuke kutumika kutenda vitendo vinavyoweza kuvuruga umoja wa kitaifa na kuhatarisha usalama wa taifa akisisitiza kuwa kama wananchi au makundi mbalimbali yatakuwa na madai au changamoto zifikishwe serikalini na kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu na sheria zilizowekwa na Serikali ipo tayari kusikiliza wote wenye madukuduku, wenye ushauri na wenye maswali, hakuna sababu ya kuharibu nchi.
Katika hatua nyingine Msigwa ameeleza kuwa athari za kuvuruga nchi zitaangukia kwa Watanzania wenyewe na sio wale wanaochochea kutoka mbali akibainisha kuwa malengo ya watu wanaotengeneza chokochoko, kufanya uchochezi mitandaoni na kwenye vyombo vya habari ni kutia hasira watu ili waiharibu nchi.