Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amerejea nchini akiwa na Tuzo maalumu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyokabidhiwa na Shrikisho la Mpira wa Mguu Barani Afrika (CAF) Novemba 19, 2025 Rabbat, Morocco ikiwa ni kutambua mchango wake katika maendeleo ya michezo nchini.
Katibu Mkuu Msigwa amewasili leo Novemba 21, 2025 ambapo kupitia tuzo hiyo, Tanzania imetambuliwa kama miongoni mwa mataifa yanayopiga hatua kubwa katika kukuza, kuimarisha na kuendeleza soka la ushindani katika ngazi za vijana, wanawake na ligi za ndani na katika mashindano makubwa yanayohusisha timu za Taifa.
Akizungumza mara baada ya kuwasili Msigwa alisema “Tuzo hiyo si ya Mhe Rais pekee yake, ni ya Watanzania wote. Na ni matokeo ya umoja, juhudi na imani katika kuendeleza michezo.
"CAF wametutambua kwa sababu tuna safari ya maendeleo inayoonekana,” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kusimamia mageuzi ya michezo, hususan kandanda, ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kupaa kimataifa na kutoa nafasi kwa vijana wenye vipaji kuonesha uwezo wao.