Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Tanzania ni Salama, Shughuli Zinaendelea
Nov 23, 2025
Tanzania ni Salama, Shughuli Zinaendelea
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza leo Novemba 23, 2025 Jijini Dar es Salaam na Waandishi wa Habari kuelezea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyotokea nchini, Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata
Na Mwandishi Wetu - Dodoma

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Tanzania ni shwari na Watanzania wanaendelea na shughuli zao kama kawaida akisisitiza kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuhakikisha watu na mali zao wanaendelea kuwa salama.

Msigwa ametoa kauli hiyo leo Novemba 23, 2025 Jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari kuelezea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa amani vilivyotokea nchini, Oktoba 29, 2025 na siku zilizofuata ambavyo vilidhibitiwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

Amesema kwa sasa shughuli za kiuchumi zinaendelea vizuri na Tanzania ni moja ya nchi chache ambazo zinakwenda kupiga hatua kubwa za kiuchumi kupitia miradi mikubwa ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa na ile inayotoa huduma.

Msigwa amesema Serikali imeendelea kuhakikisha miradi yote inatekelezwa ili kutoa ajira na kuongeza kipato kwa vijana wengi zaidi ambapo pia kupitia fursa hizo Serikali inaendelea kutangaza ajira nyingi kadri siku zinavyokwenda.

Kwa upande wa sekta ya usafirishaji, ameeleza kuwa maboresho makubwa yaliyofanywa na Serikali katika bandari ya Dar es Salaam yameogeza ufanisi wa bandari hiyo ambapo sasa uwezo wa bandari hiyo kuhudumia mizigo umeongezeka maradufu kutoka kuhudumia tani milioni 21 mpaka tani milioni 32 ndani ya miaka 3.

Aidha, mapato ya bandari hiyo pia yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 900 hadi zaidi ya shilingi Trilioni 1.8. “ Baada ya Serikali kuamua kushirikiana na DP World, uwezo wa bandari kuhudumia mizigo umeongezeka maradufu kutoka kuhudumia tani milioni 21 mpaka tani Milioni 32 ndani ya miaka 3 mapato  pia yameongezeka kutoka shilingi Bilioni 900 hadi zaidi ya shilingi Trilioni 1.8”

Msigwa ameongeza kuwa muda wa meli kusubiri kushusha shehena katika bandari ya Dar es Salaam umepungua kutoka siku 46 hadi 7 ambapo pia gharama za uendeshaji wa bandari zimeshuka na kusaidia kuokoa zaidi ya shilingi Bilioni 400 baada ya uwekezaji wa DP World.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi