Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Kuvunja Rekodi Afrika Umeme Vijijini
Jul 09, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Veronica Simba na Hafsa Omar - Mara

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuvunja rekodi kwa Marais wote wa Afrika katika uunganishaji umeme vijijini.

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amebainisha hayo wakati akizungumza na wananchi katika hafla ya uzinduzi wa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili, ngazi ya Mkoa, iliyofanyika katika Kijiji cha Kitunguruma, Kata ya Mbaribari, wilayani Serengeti, mkoani Mara, Julai 8 mwaka huu.

Akifafanua, Dkt. Kalemani alieleza kuwa Tanzania inatarajiwa kuandika historia ya kuunganisha umeme katika vijiji vyote vya Tanzania Bara ifikapo Disemba 2022 hivyo kuongoza katika Bara la Afrika kufikia mafanikio hayo.

“Tulianza utekelezaji wa miradi hii katika ngazi ya wilaya, kisha vijiji ambapo hadi sasa zaidi ya vijiji 10,312 vimeshapelekewa umeme; na vilivyobakia takribani vijiji 1,956 ndivyo vinapelekewa katika mradi huu,” alibainisha Waziri.

Akieleza zaidi, Dkt Kalemani alisema mafanikio hayo makubwa yametokana na uongozi mzuri wa Rais Samia ambaye Serikali anayoiongoza imedhamiria kwa dhati kuleta maendeleo kwa wananchi.

Awali, akielezea utekelezwaji wa Mradi huo katika Mkoa wa Mara, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Amos Maganga, alibainisha kuwa utagharimu takribani shilingi bilioni 9.63

Aidha, aliongeza kuwa Mradi umelenga kuvifikishia umeme vijiji 45 vya Mkoa huo ambavyo ndivyo pekee vilivyosalia kati ya vijiji vyake vyote 459.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mbunge wa Serengeti Amsabi Mrimi na Mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara, waliipongeza Serikali kwa kazi nzuri ya usambazaji umeme vijijini na kuahidi kuwa wananchi wao wako tayari kupokea umeme na kuutumia kwa shughuli za maendeleo.

Hafla hiyo ya uzinduzi ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi