Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Wizara ya Uchukuzi kuimarisha akiba ya kimkakati ya mafuta ili kuongeza uthabiti wa taifa dhidi ya misukosuko ya kimataifa inayoathiri bei ya nishati katika soko la dunia.
Akizungumza leo Machi 3, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa mradi wa ujenzi wa matanki ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika eneo la Kigamboni, Rais Samia amesema Tanzania haina budi kujiandaa mapema kukabili changamoto za mabadiliko ya bei yanayosababishwa na migogoro ya kimataifa.
Ameeleza kuwa misukosuko iliyojitokeza wiki iliyopita katika baadhi ya nchi tayari imechangia kupanda kwa bei ya mafuta kwa takribani asilimia 13, hali inayoweza kuathiri gharama za maisha na uendeshaji wa shughuli za kiuchumi.
“Tumuombe Mungu watu wale wakae mezani wazungumze, wakubaliane, misukosuko hii iishe ili dunia irudi katika hali yake ya kawaida ya kuendesha chumi za nchi zetu,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya kuhifadhi mafuta ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha usalama wa nishati nchini na kulinda uchumi dhidi ya athari za mabadiliko ya ghafla ya bei katika soko la kimataifa.
Aidha, ameongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kuhakikisha upatikanaji wa nishati unakuwa wa uhakika, nafuu na endelevu kwa maendeleo ya viwanda, biashara na ustawi wa wananchi.
Mradi huo wenye uwezo wa kuhifadhi mita za ujazo 374,000 ambazo ni sawa na Lita milioni 378, unatarajiwa kuongeza uwezo wa taifa kuhifadhi akiba ya kimkakati, kupunguza utegemezi wa ununuzi wa dharura na kusaidia kudhibiti mishtuko ya bei kwa walaji wa ndani.