Tanzania imeandika ukurasa mpya katika sekta ya bandari baada ya kuzindua mradi mkubwa wa ujenzi wa matenki ya kisasa ya kupokea na kuhifadhi mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam, mradi unaotajwa kuwa kichocheo kipya cha ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizindua ujenzi wa mradi huo leo Machi 3, 2026 Jijini Dar es salaam katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi, Rais wa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Ndugu viongozi na wananchi, bandari yetu ya Dar es Salaam ina mchango mkubwa sana katika kukuza uchumi wa nchi yetu na ustawi wa wananchi,” amesema Rais Samia huku akisisitiza kuwa maboresho yanayoendelea tayari yamezaa matunda.
Rais Samia amesema, mapato ya Serikali kupitia kodi ya forodha yameongezeka kwa kasi, kutoka Shilingi trilioni 7.3 mwaka 2020/2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 12.31 mwaka 2024/2025 ishara ya mafanikio ya mageuzi yanayoendelea bandarini.
Aidha, Rais Samia ametoa maelekezo kwa Wizara ya Uchukuzi kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa haraka na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) kuimaisha mfumo wa uhakiki wa ufuatiliaji ili kuongeza uwazi na uwajibikaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) , Plasduce Mkeli Mbossa, amesema mradi huo wenye thamani ya Shilingi Bilioni 678.641 unatarajiwa kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania, kupunguza siku za kushusha mizigo, kuongeza mapato, kuondoa gharama za kusubiria mafuta kwa muda mrefu bandarini na kuongeza fursa za wafanyabishara.
“Mradi huu utaleta mageuzi makubwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Kupunguza muda wa kuhudumia mizigo, kuongezeka kwa mapato ya Serikali na ajira kwa wananchi. Hii ni dalili kwamba Tanzania inaimarisha nafasi yake kama lango kuu la biashara katika ukanda huu” amesema.