Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha sekta binafsi nchini inanufaika kikamilifu na fursa zitakazotokana na Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Hayo yamejiri kufuatia kikao muhimu cha Kamati ndogo ya maandalizi ya AFCON kilichofanyika jijini Dar es Salaam kati ya Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma na uongozi wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) ukiongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu, Bw. Deogratius Masawe.
Lengo kuu kikao hicho ni kufungua mazungumzo kuhusu ushiriki wa sekta binafsi katika maandalizi ya AFCON pamoja na kujadili namna ya kuandaa mazingira wezeshi kwa wawekezeji wa ndani kuchangamkia fursa za uwekezaji, huduma na biashara kuelekea mashindano hayo makubwa barani Afrika yatakayofanyika nchini kwa ushirikiano wa nchi za Kenya na Uganda.