Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azzan Zungu na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Martin Chungong, wamesaini makubaliano yanayoliwezesha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika Oktoba, 2026 jijini Arusha.

Akizungumza mara baada ya hafla ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika katika Ofisi ndogo za Bunge Jijini Dar es Salaam leo Februari 27, 2026, Spika Zungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia Bunge kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaotarajiwa kuhudhuriwa na washiriki wapatao 2,000 kutoka mabunge wanachama 183.
Amesema kufanyika kwa mkutano huo nchini kunatoa fursa kwa wananchi hususani wa Mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla kunufaika kiuchumi kupitia biashara, chakula, malazi, usafiri na utalii.

Mhe. Zungu amesema maandalizi ya mkutano huo tayari yameanza kwa kuunda kamati maalum inayoongozwa na Katibu wa Bunge Baraka Leonard kuhakikisha mkutano unafanyika kwa kiwango cha juu.
Kwa upande wake, Chungong amesema kusainiwa kwa mkataba huu kunaonesha utayari wa pande zote mbili na ameishukuru Serikali kwa kuruhusu Tanzania kuandaa mkutano huo. Amesema ana imani kwamba Mkutano wa IPU 153 utajadili masuala muhimu na kuleta suluhisho kwa changamoto za dunia.

Hafla ya saini mkataba hiyo imefanyika katika Ofisi Ndogo za Bunge jijini Dar es Salaam na kushuhudiwa na Rais wa IPU mstaafu Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika Daniel Sillo, Balozi wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa Geneva Hoyce Temu, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Ngwaru Magembe .