Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuimarika kwa ulinzi na usalama wa Taifa ni ushahidi wa moja kwa moja wa ukuaji wa uchumi nchini.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2026 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa iliyofanyika Kikombo, wilayani Chamwino, jijini Dodoma.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema maendeleo ya kiuchumi ya Tanzania ni kiashiria tosha kwamba mazingira ya ulinzi na usalama yameimarika, akisisitiza kuwa hakuna uwekezaji unaoweza kufanyika bila kuwepo kwa mazingira salama.

“Jinsi Taifa letu linavyokuwa kiuchumi ni kiashiria kwamba hali ya ulinzi na usalama imeendelea kuimarika,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais ameeleza kuwa shirika la kimataifa la tathmini ya uchumi, Moody's, limeipatia Tanzania daraja la B1 — kiwango alichokieleza kuwa ni kizuri na chenye matumaini kwa mustakabali wa uchumi wa nchi.

Rais Samia amesisitiza kuwa uwekezaji katika sekta ya ulinzi ni jambo lisiloepukika kutokana na umuhimu wake katika kulinda mafanikio ya kiuchumi na kuhakikisha ustawi wa Taifa na wananchi kwa ujumla.

Amesema Serikali itaendelea kuliimarisha Jeshi kwa kuboresha mazingira ya kazi, vifaa na miundombinu, ili liwe tayari wakati wote kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.