Na. Thobias Robert- MAELEZO. Mfumuko wa bei za bidhaa za vyakula na sizizo za vyakula umepungua kwa mwezi Agosti kwa asilimia 5 ikilinganishwa na mwezi Julai ambao ulikuwa ni asimilia 5.2, huku Fahirisi za bei zikipungua hadi 108.46 ikilinganishwa na mwezi Julai ambayo ilikuwa ni 108.85.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii Bw. Ephraim Kwesigabo katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwa ni lengo la ofisi hiyo kuujulisha umma juu ya mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na nishati hapa nchini.
“Kupungua kwa Fahirisi za bei kwa mwezi Agosti kumechangiwa hasa na kupungua kwa bei za baadhi ya vyakula hapa nchini pamoja na baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula kama vile Dizeli pamoja na Petroli,” alifafanua Bw. Kwesigabo.
Aidha Bw. Kwesigabo, alivitaja baadhi ya Vyakula vilivyoshuka bei kwa mwezi Agosti ni pamoja na Mchele kwa asilimia 1.2, mahindi 1.2, unga wa mahindi 1.6, dagaa 3.4, mbogamboga 1.2, maharage 3.2 viazi 3.5, pamoja na ndizi za kupika 2.4.
Vilevile Bw. Kwesigabo alizitaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kushuka kwa mfumuko wa bei kuwa ni Dizeli kwa asilimia 2.2, Petroli asilimia 2.4 pamoja na vifaa vya kielektroniki kwa asimilia 1.6. lakini pia aliongeza kuwa mfumuko wa bei kwa kipimo cha mwaka kwa bidhaa za vyakula nyumbani na migahawani umepungua kwa mwezi Agosti hadi asilimia 9.1 kutoka asilimia 9.3 kwa mwezi Julai.
Bw. Kwisegabo alisema kuwa thamani ya Shilingi 100 ya Tanzania imeongezeka ikilinganishwa na mwezi uliopita ambapo alisema, “uwezo wa shilingi 100 ya Tanzania katika kununua bidhaa na huduma umefikia shilingi 92.20 mwezi Agosti, ikilinganishwa na Shilingi 91.87 ilivyokuwa mwezi Julai ya mwaka huu.”
Mkurugenzi huyo wa Sensa na Takwimu za Jamii alibainisha kuwa, mfumuko huo umepungua zaidi ikilinganishwa na nchi ya Kenya, ambapo mfumuko huo umeongeza kwa asilimia 8.04 ikilinganishwa na mwezi Julai ambao ulikuwa asilimia 7.47, kwa upande wa Uganda mfumuko wa bei umepungua sawa na Tanzania ikiwa ni asilimia 5 ikilinganishwa na 5.2 kwa mwezi Julai.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu kupitia idara yake ya Sensa na Takwimu za Jamii imekuwa na utaratibu wa kutoa takwimu za mwenendo wa bei za vitu mbalimbali hapa nchini kila mwisho wa mwezi ili kuwafahamisha watanzania.