Na Judith Mhina-MAELEZO
Wilaya ya Mtwara ndiyo lango linalofungua maendeleo wa uchumi wa Kusini mwa Tanzania kwa kuunganisha mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma ikiwa ni pamoja na nchi jirani za Malawi, Msumbiji na Zambia zitakazowezeshwa kwa sehemu kubwa kusafirisha mizigo yao kwa urahisi kupitia bandari ya Mtwara.
Wilaya hiyo, imejipambanua kutokana na uwepo wa gesi ya asili, ugunduzi wa mafuta kwenye ukanda wa bahari, uwepo wa lango kuu la bandari ya Mtwara na barabara za kiuchumi ikiwemo ya Mtwara-Masasi – Songea, itakayosafirisha madini ya chuma na makaa wa mawe kutoka Liganga, Mchuchuma, Ngaka na Kiwira pamoja na mazao ya kimkakati kama korosho na ufuta ambapo shughuli zote hizo zitakuwa chanzo na chachu ya kuimarisha maendeleo ya uchumi wa Kusini.
Hayo amesema Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Dastun Kyobya alipofanya mahojiano na Idara ya Habari- Maelezo ofisini kwake hivi karibuni, ambapo ameonyesha ni kwa jinsi gani Wilaya ya Mtwara yenye Tarafa nane, Kata 56, Vitongoji 744, Vijiji 197, na Mitaa 120 ndani ya halmashauri tatu za Mtwara Mikindani, Nanyamba na Mtwara Vijijini zinazoboresha uchumi wa lango la kanda ya Kusini. Kwa namna moja au nyingine kuboreshwa kwa bandari, miundombinu ya barabara, umeme wa gesi, ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda kumeimarisha fursa kwa wilaya hiyo kuwa lango kuu la kuendeleza maendeleo ya uchumi wa Mtwara corridor kupitia miradi ya Export Processing Zone (EPZ) na Special Economic Zone (SEZ).
Kyobya amesema “Maboresho yaliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli, katika Wilaya yetu yameinua hadhi ya wilaya hii ambayo ni kiungo kikubwa katika uchumi na uwekezaji hususan viwanda vya korosho, mabibo na biashara ya utalii, ambayo tunahakika itaboresha maisha ya Watanzania na kutoa huduma kwa nchi jirani zisizo na bahari yaani Malawi, Msumbiji na Zambia”.
Akionyesha vichocheo vya kufanikisha azma ya Serikali ya kuhakikisha maendeleo na uchumi wa Mtwara corridor inafanikiwa amesema kuwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mitego ambayo inawahakikishia afya wawekezaji, wafanyabiashara, watalii wa ndani na nje na Watanzania wa mikoa ya kusini, kuwa wako salama zaidi kiafya kwa kuwa huduma zote za uhakika zipo na zinapatikana wakati wanapozihitaji jambo litakalovutia zaidi katika kuimarisha uchumi wa eneo maalum la uwekezaji la Kusini.
Akielezea barabara za uchumi, Kyobya amesema kuwa barabara ya Mtwara- Mrivata ya kilometa 50 ambayo inapita katika Wilaya za kimkakati zinazozalisha korosho kwa wingi za Newala, Tandahimba na Masasi itagharimu shilingi bilioni 89,591,008,355.00. Barabara hiyo itakuwa na upana wa mita 9.5 ambapo mita 6.5 ni njia ya magari na mita 1.5 kila upande ni mabega ya barabara ambapo itahusisha makaravati makubwa sita na madogo 44. Ujenzi huu umetanguliwa na usanifu wa kina uliogharimu shilingi bilioni 1.280,831,600.00 na gharama ya mshauri mwelekezi anayesimamia ujenzi kwa gharama shilingi bilioni 5,065,054,871.01 ambapo kutokana na ujenzi wa barabara hii jumla ya shilingi milioni 70,435,260.94 zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa barabara.
Akiongelea suala la umeme wa uhakika kutokana na uwekezaj mkubwa utakaofanyika katika Wilaya ya Mtwara na maeneo mengine husika, Kyobya amesema kuwa umeme unaotumika katika eneo lake umetokana na gesi inayochakatwa katika kiwanda cha gesi Madimba hivyo bila shaka yeyote suala zima la maendeleo ya uchumi ya eneo la Kusini limefanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Taarifa iliyopatikana kutoka Bandari Mtwara imesema kuwa bandari hiyo imepanuliwa kwa gharama ya shilingi bilioni 137,385,612,736.78 ambapo imeongeza vifaa vya kuhudumia shehena pamoja na kupanua miundombinu kwa kufanya ujenzi wa gati wenye uerefu wa mita 300 kina mita 13CD na yadi ya makasha (container yard) inayotarajiwa kuwa na mita za mraba 79,000 ambapo ikikamilika itakuwa na uwezo wa kuhudumia meli zenye uwezo wa kubeba tani 65,000 DWT, ikiwa ni pamoja na kuhudumia shehena tani 1,000,000 kwa mwaka kutoka shehena 400,000 za awali.
Aidha,taarifa hiyo imeongeza kuwa pamoja na ujenzi huo, bandari inaendelea na ujenzi wa yadi ya mita za mraba 5,600, ukarabati wa ghala namba tatu la kuhifadhi mizigo, ujenzi wa dira ya kupimia mafuta. Aidha ununuzi wa vifaa uliofanyika ni pamoja na terminal tractors pamoja na matela yake sita skid steers mbili na hoppers mbili.
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua kuwa shughuli za ujenzi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na utengenezaji wa precast beams ambao umefikia asilimia 98, pre-cast slab za zege kwa ajili ya sakafu ya gati asilimia 73, usimikaji wa nguzo za gati asilimia 88, ujenzi wa kofia za nguzo asilimia 71, ujenzi wa safu ya mawe ukingo (revetment ) asilimia 33, ujenzi wa yadi kwa zege (CBM3) asilimia 21, usimikaji na uunganishaji (wet joint) kwa precast beams na pre cast slab asilimia 15, pamoja na ujenzi wa miundombinu saidizi ya huduma kama maji safi, maji taka mifumo ya zimamoto, uzio, geti na mifumo ya umeme imefikia asilimia 38.
Faida ambazo Watanzania wamezipata kutokana na mradi huo ni pamoja na ajira za wazawa ambapo meneja wa mradi, mkadiriaji majenzi, mtaalamu wa mazingira na mkandarasi walioajiriwa ni wazawa katika kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na watu 308, sawa na asilimia 87.5 ya wafanyakazi wote. Kampuni za wazawa zaidi ya 30 zimetoa huduma mbalimbali katika mahitaji ya kokoto, saruji, mchanga nondo, udongo pamoja na vipuli vya mitambo vya ujenzi.
Upande wa Mshauri mwelekezi ni raia wa Ujerumani, lakini wahandisi wote 10 wanaosimamia shughuli za kila siku pamoja na wafanyakazi saba wa kada nyingine ni wazawa.
Pamoja na kuendelea kwa upanuzi wa Bandari ya Mtwara, mkoa huo pia unaendelea na upanuzi wa uwanja wa ndege ili kuwa na uwanja bora na wa kisasa utakaowawezesha wageni,watalii,wafanyabiashara na wawekezaji kufika mkoani humo kwa urahisi.
Mhandisi wa ujenzi wa Mkoa wa Mtwara, Dotto John amesema “Upanuzi wa uwanja wa ndege ambao upo katika Wilaya ya Mtwara utawezesha ndege kubwa kutua moja kwa moja mtwara badala ya Dar-es-salaam ambapo wafanyabiashara na wawekezaji watavutiwa zaidi huduma inapokuwa mahali husika. Hivyo upanuzi unaofanyika ni njia ya kurukia ndege kutoka upana wa mita 30 na kuwa mita 45, na kujenga upya matabaka ya kurukia na kutua kwa viwango vya matabaka matano tofauti hadi tabaka la lami imara yenye unene wa 100 milimita”.
Aidha, amezitaja kazi nyingine zilizofanyika kuwa ni pamoja na kuongeza barabara ya kurukia na kutua ndege kutoka mita 2,258 za sasa hadi mita 2,800, kujenga maegesho mapya ya ndege (Apron) katika eneo jipya la master plan, kujenga barabara moja ya kiungio yaani (taxiway) katika eneo jipya la master plan. Vile vile kazi zinazotegemewa kuanza muda wowote kuanzia sasa ni kujenga barabara ya magari ya kuingia kiwanjani pamoja na maegesho ya magari, kujenga na kuimarisha maeneo ya usalama kiwanjani (runway strip), kuweka vifaa vya zimamoto na kuweka matenki ya kuhifadhi maji yenye uwezo wa kuchukua mita za ujazo 200, kuweka taa pamoja na alama za kuongezea ndege kujenga uzio wa usalama kuzunguka kiwanja na kuweka mfumo wa umeme wa akiba.
Juhudi kubwa za uwekezaji na uboreshaji zilizofanya na Serikali ya Awamu ya Tano katika mkoa huo katika nyanja mbalimbali zitauwezesha kuimarika kiuchumi na kiutalii hasa kutokana na kuwa na fursa mbalimbali za umeme wa gesi utakaochochea uendelezaji wa ujenzi wa viwanda, uwepo wa utajiri mkubwa wa makaa ya mawe pamoja na uwepo wa mazao ya kimkakati ya korosho na ufuta.
Mradi wa Maendeleo wa Mtwara Corridor umeanzishwa kwa madhumuni ya kuendeleza miundombinu ya Kusini mwa Tanzania ili kuweza kuwa kiungo muhimu na upande wa Kaskazini mwa Msumbiji na upande wa Mashariki wa Malawi na Zambia. Lengo la mradi huu ni uwepo wa barabara za uhakika, reli, na njia za majini (bandari ya Mbamba Bay kwenye Ziwa Nyasa) na za uhakika katika ukanda wa Mtwara kuunganisha na Corridor ya Malawi na barabara itakayounganisha Malawi kuelekea Msumbji ili kukuza uchumi na kuleta maendeleo kwa watu husika.
Wazo hilo lilianza mwaka 2000 kwa viongozi wanne wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Tanzania (SADC) na mwaka 2004 viongozi wakuu wa nchi za Tanzania Benjamin Mkapa, Msumbiji Joachim Chisano, Malawi Bingu wa Mutharika na Zambia Levy Mwanawasa walisaini mkataba wa kufanya Mradi wa Maendeleo wa Mtwara Corridor kuwa kweli na wala sio ndoto kwa kujenga daraja la Umoja la mto Ruvuma pamoja na barabara za kuunganisha Malawi, ziwa Nyasa na Mbinga kuelekea Bandari ya Mbamba Bay.
Ndoto hiyo imetimia kwa kujengwa barabara kutoka bandari ya Mtwara mpaka Songea yenye takriban kilometa 804 na barabara ya Mbinga kuelekea Mbamba Bay inakadiriwa kukamilika mwaka huu wa fedha 2020/2021 yenye urefu wa kilometa 67 Ndoto hiyo ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Rais Samora Macheal wa Msumbiji ilitimizwa na Rais wa Awamu ya Tatu Mheshimiwa Benjamin Willium Mkapa mwaka 2010 kwa kujenga daraja la Umoja lililounganisha Tanzania na Msumbiji kupitia Mto Ruvuma, ambapo Msumbiji wameendelea kujenga barabara ya kilometa 175 ya Negimano mpaka Mueda inayounganisha corridor hiyo na barabara kuu za Msumbiji.