Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Dkt. Kalemani Azindua Ulipaji Fidia Bomba la Mafuta
Jul 08, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Hafsa Omar-Tabora

Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi ulipaji wa fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP).

Tukio hilo limefanyika Julai 7, 2021, katika kijiji cha Sojo, kata ya Igusule, Wilaya ya Nzega, Mkoani Tabora.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Kheri Mahimbali, Mkuu wa Mkoa wa Tabora Batilda Buriani, Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Nishati na Madini, viongozi mbalimbali wa Wizara na Taasisi zake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kalemani amesema zoezi la kulipa fidia kwa wale wote ambao wanastahili kupata fidia limeanza rasmi na watu wote watafidiwa kwa usahihi na kwa wakati.

“Kwa sababu Serikali ni sikivu na inawajali wananchi wake wote ambao watafikiwa kwa namna yoyote ile na mradi huo wote watafidiwa kwasababu Serikali imetoa fedha za kutosha kwa ajili ya malipo,” alisema Mhe. Kalemani.

Aidha, Waziri wa Nishati amesema gharama za fidia katika mradi mzima kutoka kyaka Mkoani kagera hadi Chongoleani Mkoani Tanga ni shilingi bilioni 28.26 za Kitanzania.

Amesema Serikali imeamua kuzindua ulipaji wa fidia katika kijiji cha Sojo kwasababu eneo hilo lipo katikati baina ya Hoima Uganda na chongeleani Tanga na kuwataka wasimamizi wa mradi huo kujenga karakana katika eneo hilo kwakuwa karakana zinajengwa katikati ya mradi.

Dkt. Kalemani ameeleza kuwa, wanufaika wa mradi huo watakuwa Watanzania wote kwa jumla lakini waliopitiwa na mradi watanufaika zaidi kwa sababu fursa mbalimbali zitapatikana wakati wa ujenzi wa mradi katika maeneo yao na kuwataka wananchi hao kujitokeza kwenye kuchukua fursa mbalimbali za mradi.

Pia, amesema kutokana eneo hilo ndio linatumika kujenga kambi, wananchi wa eneo hilo watafaidika na ujenzi wa huduma za kijamii kama vile  kituo cha  afya, Shule na barabara ambazo zitajengwa mara baada ya ujenzi wa mradi kuanza.

Dkt. Kalemani, amewataka wananchi ambao watalipwa fidia zao kuanza kuondoka kwenye maeneo hayo ili ujenzi wa mradi uanze mara moja.

“Ukishalipwa na pesa umepewa na ni haki yako, basi pisha mradi asije akatokea mtu akalipwa halafu akazitumia pesa zote baadae akasema pesa alizolipwa ni ndogo, kwa hiyo tuheshimu malipo ya fidia na tuzitumie pesa kwaajili ya maendeleo,”alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Dkt. James Mataragio, amesema zoezi la ulipaji fidia lipo tayari kuanza kwa maeneo yote 12 ambapo timu za wawakilishi wa Serikali, wawakilishi wa Kampuni ya EACOP, Kampuni ya Uthamini (White Night) na Kampuni ya Ushirikishaji na Kusaidia Jamii (JSB) zipo katika baadhi ya Mikoa wakitekeleza shughuli za zoezi hilo.

Amesema, utwaaji wa ardhi umezingatia Sheria na Kanuni za ndani za uthamini na utwaaji wa ardhi, vilevile ili Mradi  uweze kukidhi vigezo vya kupata mikopo ya kimataifa, kumekuwepo na nyongeza ya manufaa mbalimbali kwa wananchi waliopisha mradi ikiwemo nyongeza ya fidia, kujengewa nyumba mbadala  za kisasa.

Dkt. Mataragio ameongeza kuwa, mara tu baada kukamilika kwa taratibu jumla ya wananchi 391 waliopisha mradi watalipwa fidia ambapo wananchi waliopisha Mradi wapatao 44 wametoka kijiji cha Sojo ambao baadhi yao leo hii watasaini mikataba ya kulipwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi