Na Oscar Assenga - Pangani
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Captain Mussa Mandia ametoa wito kwa wavuvi na wasafirishaji Kata ya Kipumbwi wilayani Pangani mkoani Tanga kuacha kutumia vyombo vya kubebea mizigo kwa ajili ya kusafiria badala yake watumie vile vilivyoruhusiwa kisheria.
Hatua hiyo inatokana na eneo la Kipumbwi kushamiri vitendo vya abiria na mizigo kupanda kwenye vyombo vya kusafirishia mizigo kufanya safari zao kati ya Kipumbwi kuelekea Visiwa vya Unguja na Pemba na hivyo kuhatarisha usalama wa maisha yao na mali.
Captain Mandia aliyasema hayo wakati wa ziara ya kuitambulisha Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika hilo ambao wapo mkoani Tanga na walianzia kwa kutembelea Bandari ya Tanga na maeneo mengine lengo ni kusikia changamoto walizonazo kwenye eneo la kipumbwi na kuona namna ya kuzifanyia kazi.
Alisema kwao kama Shirika wanasimamia ulinzi na usalama wa usafiri majini hivyo Serikali itachukua njia nzuri za usafiri bila kupoteza maisha na mali zenu hivyo alihaidi kulichukua suala hilo na kuhakikisha linafanyiwa kazi.
“Sisi kama Shirika jukumu letu ni kusimamia ulinzi na usalama, niwaahidi suala la chombo cha usafiri hapa Kipumbwi tunalichukua na kuona namna linafanyiwa kazi”, alisema.
“Hata leo asubuhi wakati nazungumza na Mkuu wa Wilaya ya Pangani nimemueleza tutakachofanya kwa mamlaka tulionayo ni kuangalia namna ya kuboresha sheria, kanuni na taratibu tulizonazo kufikia mahali ambapo kutakuwa na vyombo vizuri kwa ajili ya kusafisha watu”, alisema Captain Mandia
Hata hivyo aliwaambia wananchi wa eneo hilo kwamba kilio chao kimefika Serikalini na watalifanyia kazi ili kuona namna ya kulipatia ufumbuzi kwa lengo la kuondosha changamoto iliyopo.
Akizungumzia suala la Light House kwenye eneo hilo, Captain Mandia alisema kwamba wao Shirika wanajukumu la kudhibiti vyombo vya usafiri hivyo watawaelekeza Bandari kwamba kila wanaporasimisha wajitahidi kuhakikisha kuweka vitu ambavyo vinahitajika ili kuwasaidia wananchi ikiwemo kuweka (Light Huose) Taa,
Alisema taa hizo ambazo zitakuwa zikiwaka zitakuwa zikiashiria eneo husika ili kuweza kuwaepusha kupotea wanapokuwa majini wakiendelea na shughuli za uvuvi.
Kuhusu chombo cha uokoaji alisema tayari wao TASAC wanakuja na utaratibu huo na inategemea na bajeti maana nchi inasehemu kubwa sana ya maji hivyo wamelichukua na kuona namna ya kulifanyia kazi.