Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Wizara ya Ardhi Yaja na Mabadiliko Makubwa ya Kimfumo
Aug 31, 2023
Wizara ya Ardhi Yaja na Mabadiliko Makubwa ya Kimfumo
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga akizindua zoezi la kuondoa mlundikanao wa mashauri ya ardhi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, uzinduzi uliofanyika wilayani Bagamoyo iliyopo katika Mkoa wa Pwani tarehe 31 Agosti, 2023.
Na Na Munir Shemweta, WANMM, Bagamoyo

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaendelea kufanya maboresho makubwa ya kimfumo na muundo kwa lengo la kuwezesha mambo mengi ya wizara hiyo kufanyika kimfumo,

Hayo yamebainishwa leo tarehe 31 Agosti, 2023 na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga wakati akizindua zoezi la kuondoa mlundikano wa mashauri katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya, uzinduzi uliofanyika wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.

Amesema, kumekuwa na changamoto kubwa hasa wananchi wa kawaida wanapokwenda ofisi za ardhi kupata namba ya malipo (Control number) hivyo wizara inakuja na mfumo utakaomuwezesha mwananchi kupata namba hiyo ya malipo mwenyewe.

“Kumekuwa na changamoto kubwa hasa wananchi wetu wa kawaida wanapokwenda ofisi zetu za ardhi kupata tu control namba inakuwa changamoto, inakuwa kama biashara sasa tunakuja na mfumo utakaomuwezesha mwananchi kupata control number mwenyewe”, alisema Mhandisi Sanga.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, hata suala la kufanya utafiti kwa wananchi wanaotaka kununua nyumba au kiwanja nalo anaweza kufanya mwenyewe ambapo kwa sasa analazimika kutoa fedha ili kufanyiwa.

“Mnafahamu mtu akitaka kununua nyumba au kiwanja cha mtu katika kufanya upekuzi anaambiwa pia alipe shilingi 40,000 au 100,000 afanyiwe haraka haraka nayo pia tunaenda kukomesha, mwananchi atafanya upekuzi mwenyewe”, alisema Mhandisi Sanga.

Sehemu ya washiriki wa uzinduzi wa zoezi la kuondoa mlundikano wa mashauri ya ardhi katika Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya uliofanyika Bagamoyo Mkoa wa Pwani tarehe 31 Agosti, 2023.

Aliongeza kwa kusema, kubwa zaidi katika maboresho hayo ni suala la kulipia kodi ya pango la ardhi ambapo kazi yake inakwenda kukamilika hivi karibuni hivyo wananchi wataweza kulipia kupitia simu ya mkononi sambamba na kupata bili kama wanavyopata katika maji.

“Utakapokuwa na namba ya NIDA utapata mambo yote, katika wizara yetu ya ardhi wamelizingatia agizo la Mhe. Rais ambapo kwa kutumia kitambulisho cha NIDA mwananchi atapata taarifa zote kuhusina na masuala ya ardhi”, alisema Mhandisi Sanga.

Akigeukia zoezi la kuondoa mlundikano wa mashauri ya ardhi, amesema zoezi hilo ambalo uzinduzi wake umefanyika pia kwenye wilaya za Musoma, Tarime, Ifakara pamoja na Tabora, katika kipindi cha mwezi mmoja jumla ya mashauri 500 yanatarajiwa kusikilizwa na kutolewa maamuzi.

“Katika kipindi takriban siku nane toka kuanza kwa zoezi hili, Wenyeviti wameweza kusikiliza mashauri 243 katika Mabaraza niliyoyataja ambayo zoezi hilo linaendeshwa”, alisema Mhandisi Sanga.

Kwa upande wake Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini, Stela Tullo ameishukuru Wizara ya Ardhi kupitia Mradi wa Uboreshaji Miliki za Ardhi kwa kuyawezesha Mabaraza kuhakikisha yale yanayoelemewa na migogoro angalau yanapata msaada wa Wenyeviti kwenda kwenye mabaraza yenye mashauri mengi na kuyakalia vikao maalum kwa lengo la kusikilizwa na kutolewa maamuzi kwa wakati na haki.
 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi