Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza ahadi kwa vitendo, baada ya ndani ya siku 100 za muhula wa pili kufanikisha kuunganisha wilaya 10 mpya kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, hatua inayoimarisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Hayo yamebainishwa leo Februari 4, 2026 na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa ahadi za Rais Samia ndani ya Siku 100 katika Wizara hiyo.

Amesema wilaya zilizounganishwa ndani ya kipindi hicho ni Kilwa, Maswa, Bariadi, Sikonge, Urambo, Ushirombo, Chunya, Karagwe, Nzega na Butiama, mafanikio yanayodhihirisha utekelezaji wa vitendo wa ahadi za Rais Samia katika kujenga uchumi wa kidijitali.
Waziri huyo amesema kupitia uunganishwaji huo, wananchi wa wilaya husika sasa wanapata fursa za huduma bora za mawasiliano, intaneti ya uhakika, biashara mtandao, elimu ya kidijitali pamoja na huduma za afya kwa njia ya TEHAMA, hali inayopunguza pengo la kidijitali kati ya mijini na vijijini.
Utekelezaji huu umeongeza idadi ya wilaya zilizounganishwa kwenye Mkongo wa Taifa kufikia 119 kati ya wilaya 139 nchini, sawa na asilimia 86, hatua inayothibitisha kasi ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano kama nyenzo ya maendeleo endelevu.

Mhe. Kairuki ameongeza kuwa wilaya 20 zilizosalia zipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji, na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni, 2026, jambo litakaloiwezesha Tanzania kuwa na mtandao wa mawasiliano unaogusa maeneo yote ya nchi.
Amesisitiza kuwa mafanikio hayo ya kuzifikia wilaya 10 ndani ya siku 100 ni ushahidi wa dhamira ya dhati ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha kila Mtanzania ananufaika na mapinduzi ya kidijitali, huku Serikali ikiendelea kutumia miundombinu ya mawasiliano kama chachu ya maendeleo, ushindani wa kiuchumi na ustawi wa wananchi.