Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Taifa wa kuhifadhi mazingira na kulinda afya ya wananchi, hususan wanawake na watoto.
Kauli hiyo imetolewa leo Februari 4, 2024 jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mradi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Shule ya Sekondari Bunge.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Makamba amesema juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali zimeanza kuzaa matunda, ambapo matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita.

“Matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini yameongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi kufikia asilimia 23.2 mwaka 2025. Haya ni mafanikio makubwa yanayoonesha dhamira ya Serikali katika kuboresha afya za wananchi na kulinda mazingira yetu,” amesema Mhe. Makamba.

Ameeleza kuwa mafanikio hayo yametokana na utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia, juhudi za uhamasishaji kwa jamii pamoja na ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika kuhakikisha teknolojia za nishati safi zinawafikia wananchi wengi zaidi.

Aidha, Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa Wizara ya Fedha kuongeza mchango na uwekezaji katika miradi ya nishati safi, hususan katika miundombinu na utoaji wa ruzuku zitakazowawezesha wananchi wengi kumudu gharama za nishati hiyo. Vilevile, amewahimiza wazalishaji na wasambazaji wa gesi kuongeza jitihada za kusambaza huduma hiyo katika mikoa yote ya nchi, ikiwemo maeneo ya vijijini.

“Ni muhimu Wizara ya Fedha ikaendelea kuunga mkono jitihada hizi kwa kuweka rasilimali za kutosha, huku wadau wa gesi wakihakikisha upatikanaji wa nishati safi unafika katika kila mkoa ili Watanzania wote wanufaike bila kuachwa nyuma,” ameongeza.

Kwa upande wake, uongozi wa Shule ya Sekondari Bunge umeishukuru Serikali kwa kuanzisha mradi huo, ukisema utaimarisha afya ya wanafunzi na walimu, kupunguza athari za matumizi ya kuni na mkaa, pamoja na kujenga uelewa wa matumizi ya nishati safi kwa kizazi kijacho.