Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Angela Kairuki amesema ndani ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, Serikali imetenga zaidi ya Shilingi Bil. 5 kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya biashara ndogo za kati za teknolojia ya habari na mawasiliano
Amesema fedha hizo ni miongoni mwa ahadi 13 za Rais wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 ambapo, kati ya ahadi hizo, ahadi 3 zilikuwa zinaigusa wizara hiyo ikiwepo ya utoaji wa mitaji kwa ajili ya kuwezesha biashara za teknolojia ya habari.
Ameyasema hayo leo February 04, 2026 wakati akizungumza na Wananchi kupitia vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa Kipindi chake cha pili cha Serikali ya awamu ya sita

"Mheshimiwa Rais alitoa ahadi 13 ambapo kati ya hizo wizara yetu ineguswa na ahadi tatu, ambazo ni kuwezesha upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya kuwezesha Biashara ndogo za kati na uendeshaji wa kampuni changa ( startups), Mheshimiwa Rais ametekeleza ahadi hii kwa kishindo ambapo hadi kufika January 2026, Wizara imetengewa na Serikali Sh. Bil 5 kwa ajili ya mitaji ya startups

Amesema fedha hizo zitatolewa kupitia Benki za Biashara kwa kampuni changa 50 ambazo zitakuwa zimekidhi vigezo vilivyowekwa kupitia mwongozo ulioandaliwa kwa utoaji wa mkopo wa fedha hizo
Amezitaja shughuli ambazo zinanufaisha kampuni hizo changa 50 ni pamoja na maeneo ya fedha, ubunifu katika sheria, kupanga matukio, afya, akili unde, kilimo, utalii, bima, elimu na lishe.

Aidha amesema kwa sasa Wizara hiyo inaendelea kukamilisha makubaliano yake na Benki za Biashara ambapo wapo katika hatua ya mwisho kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo yenye riba nafuu kwa kampuni hizo changa 50 ambazo wataanza nazo.