Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani amekutana na washirika wa maendeleo wanaofadhili miradi ya nishati ili kujadiliana nao kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo miradi wanayoifadhili na miradi mipya inayohitaji fedha za uwekezaji.
Kikao hicho kimefanyika jijini Dodoma katika Ofisi za Wizara ya Nishati na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Katibu Mkuu wa Wizara, Dkt Hamisi Mwinyimvua, Kaimu Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Kaimu Kamishna wa Petroli na Gesi na watendaji kutoka Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Baadhi ya washirika wa maendeleo waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU), Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Benki ya Dunia (WB), Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), Ubalozi wa Ujerumani na Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania.
“Serikali haiwezi kufanya kazi peke yake hasa katika kutekeleza mipango ya muda mrefu ya kuzalisha megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025 na mipango ya muda mfupi ya kuzalisha megawati 5000 ifikapo mwaka 2020,” amesema Dkt. Kalemani.
Amesema kuwa, washirika hao wanahitajika katika kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya usambazaji na usafirishaji umeme ambapo ameeleza kuwa sehemu kubwa ya nchi ina miundombinu ya umeme ya kV 33 na 132kV lakini kwa sasa msisitizo unawekwa katika kupata fedha ya kujenga miundombinu ya msongo wa kV 220 hadi kV 400 ili kupeleka umeme mwingi na wa uhakika kwa wananchi.
Ameongeza kuwa, kwa sasa uwezo wa mitambo ya kufua umeme ni megawati 1500 lakini bado inahitajika mitambo itakayozalisha megawati 3500 ili kuweza kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka 2020, hivyo zinahitajika juhudi za pande zote mbili ili kuweza kufikia lengo husika.
Dkt Kalemani pia, amewaeleza washirika hao kuwa, Tanzania bado ina fursa za uwekezaji katika uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji ambapo kuna vyanzo vya maji vinavyoweza kuzalisha megawati 4700 lakini kwa sasa zinazalishwa megawati chini ya 600 kwa kutumia chanzo hicho.
Kuhusu umeme wa makaa ya mawe amesema kuwa, Tanzania ina mashapo ya makaa ya mawe ya kiasi cha tani 1.2 bilioni lakini hazijaanza kuzalisha umeme hivyo eneo hilo pia linahitaji ushirikiano ili makaa hayo yatumike katika kuzalisha umeme.
Aidha, amewaeleza washirika wa maendeleo kuwa, Tanzania ina upepo wenye kasi ya 8-9 kilometa kwa sekunde ambao unaweza kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 5000 lakini kwa sasa umeme wa upepo unaozalishwa nchini ni chini ya megawati 1.
Vilevile amewaeleza kuhusu fursa za uwekezaji katika uzalishaji umeme kwa kutumia Jotoardhi na kusema kuwa nchi inaweza kuzalisha umeme wa megawati 5000 kutokana na chanzo hicho ambacho hakijaanza kutumika tofauti na nchi ya Kenya ambayo inazalisha takriban megawati 200.
Kwa ujumla, Waziri wa Nishati amewaeleza Washirika hao wa maendeleo kuhusu maeneo yote yanayohitaji ushirikiano ambayo ni miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme na kuongeza ujuzi kwa wataalam nchini.
Akizungumza kwa niaba ya washirika hao wa maendeleo, Mwakilishi kutoka Umoja wa Ulaya, Jenny Correia Nunes, amemshukuru Waziri wa Nishati kwa kuitisha kikao hicho ambacho kimejenga uelewa wa pamoja kati ya pande hizo mbili na kushauri kuwa utaratibu wa vikao vya pamoja uwe ni endelevu.