Wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inajivunia mabadiliko makubwa katika Sekta zake zote ikiwemo ya habari kwa mazingira wezeshi ya kufanya kazi kwa uhuru, uwazi na kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya habari.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Palamagamba Kabudi leo Mei 7, 2025 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo Bungeni jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
“Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limepata mafanikio makubwa yakujivunia katika nyanja za habari, utangazaji, mifumo, rasilimaliwatu, upanuzi wa usikivu, ujenzi wa makao Makuu ya TBC jijini Dodoma, uanzishwaji wa chaneli za kimkakati, uboreshaji wa maslahi ya watumishi na upelekaji wa habari za nchi kimataifa hivyo kutimiza lengo kuu la kuitangaza nchi Kimataifa” amesema Waziri Prof.Kabudi.
Akieleza zaidi kuhusu mafanikio kwa upande wa michezo Prof. Kabudi amesema juhudi za maksudi za Rais wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan zimekuwa chachu ya mafanikio kwa timu za Taifa na vilabu vya ndani katika mashindano ya kimataifa ambapo kwa mara ya kwanza, baada ya miaka 30 jumla ya timu Sita (6) za Taifa zimeweza kufuzu mashindano makubwa.
“Tanzania kama mwenyeji imefuzu katika Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027) na CHAN 2024; timu ya Taifa ya wanawake imefuzu katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika la Wanawake la CAF (WAFCON) yatakayofanyika nchini Morocco; timu ya Taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Boys) ilifuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana (AFCON U-17), timu ya vijana wa umri chini ya miaka 20 imefuzu mashindano ya AFCON, 2025, timu Taifa ya mpira wa miguu imefanikiwa kufuzu katika mashindano ya AFCON, 2024 na timu ya Taifa ya Wanawake ya Futsal imefanikiwa kufuzu katika fainali za AFCON (Women’s Futsal Cup of Nations 2025) pamoja na kukata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia 2025” Amesema Waziri Prof.Kabudi.
Kwa sekta ya Sanaa Serikali ya awamu ya sita imefufua Mfuko wa Utamaduni na Sanaa uliokuwa haufanyi kazi kwa zaidi ya miaka 10 na kwa kipindi kifupi jumla ya miradi 359 ya utamaduni na Sanaa imepatiwa mikopo yenye jumla ya thamani ya Shilingi 5,250,070,500.
“Aidha, Mheshimiwa Rais amekuwa mshiriki wa moja kwa moja katika matukio na shughuli mbalimbali za Sekta zetu, ikiwemo ushiriki wake kama mgeni rasmi katika Tuzo za Ucheshi Tanzania (Tanzania Comedy Awards) zilizofanyika tarehe 22 Februari, 2025 na Tamasha la Utamaduni lililofanyika mkoani Ruvuma, tarehe 20 hadi 23, Septemba, 2024” amesema Waziri Prof. Kabudi.
Kadhalika, Waziri Kabudi imetambua mchango wa Washirika wa Maendeleo na wadau wengine wakiwemo mashirikisho, vyama, vilabu na kila mdau mmoja mmoja kwa nafasi yake ya kuhakikisha sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo zinafikia malengo yaliyokusudiwa kwa mujibu wa Sera.
Waziri Prof.Kabudi amesisitiza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika katika sekta hizi yametokana na ushirikiano miongoni mwa wadau wa Wizara wakiwemo viongozi na watumishi wa Wizara.