Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli nchini (PURA) imefanikiwa kuokoa na kurejesha shilingi Bilioni 340 kwenye mfuko wa ugawanaji wa mapato kati ya serikali na wawekezaji wa vitalu vya gesi asilia kufuatia ukaguzi wa mikataba.
Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema hayo Mei 19, 2025 wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita kwenye mkutano na Wahariri wa vyombo vya Habari jijini Dar es Salaam.
Mhandisi Sangweni alisema PURA imeendelea kuhakiki na kukagua mapato na gharama za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji katika mikataba ya ugawanaji mapato kati ya serikali na waendeshaji wa vitalu (PSA Auditing).
“Kupitia kaguzi, zaidi ya shilingi Bilioni 340 zimerejeshwa kwenye mfuko wa ugawanaji mapato kati ya serikali na wawekezaji katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita. Fedha hizi zingeweza kutumika kama marejesho ya mtaji wa mwekezaji” alisema Mhandisi Sangweni.
Kuhusu kuongezeka kwa uzalishaji wa gesi asilia, Mhandisi Sangweni alisema ndani ya miaka minne ya Rais Samia Suluhu Hassan (2021 hadi 2025) kiasi cha gesi asilia kilichozalishwa kimefikia futi za ujazo Bilioni 301.3 kati ya hizo kitalu cha Mnazi Bay kimezalisha futi za ujazo Bilioni 142.35 na Songosongo Bilioni 158.59
Mhandisi Sangweni alieleza kuwa, gesi asilia inayozalishwa inatumika kwa matumizi ya uzalishaji umeme, matumizi ya viwandani , majumbani , taasisi na katika magari.
Kuhusu ushiriki wa Watanzania na watoa huduma katika utekelezaji wa miradi ya utafutaji na uzalishaji wa gesi asilia, Mhandisi Sangweni alisema PURA imeendelea kusimamia Sheria ili kuhakikisha nchi inanufaika na rasilimali zake.
Aidha, PURA inaratibu mazungumzo ya utekelezaji wa mradi wa usindikaji wa gesi asilia kuwa katika hali ya kimiminika (LNG project) utakojengwa mkoani Lindi ambao utalipatia taifa manufaa ikiwemo fedha, ajira na uanzishwaji wa viwanda vinavyotumia gesi kama malighafi.
Mkurugenzi huyo aliongeza kusema kwa sasa ushiriki wa Watanzania katika ajira umefikia wastani wa asilimi 85 ikilinganishwa na asilimia 50 miaka minne iliyopita huku manunuzi ya biadhaa za ndani yamekuwa kutoka asilimia 40 hadi asilimia 60 mwaka huu.
Mkutano wa Wahariri na Wakuu wa Mashirika ya Umma umeandaliwa na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Jukwaa la Wahariri (TEF) na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali kwa lengo la kutoa taarifa za mafanikio ya taasisi za umma kuhusu miaka minne ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.