Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mfumo wa AMIS na TAUSI Kurahisisha Kazi za Sanaa Nchini
May 20, 2025
Mfumo wa AMIS na TAUSI Kurahisisha Kazi za Sanaa Nchini
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma akizungumza wakati akijibu swali la Mhe. Lucy Sabu Mbunge wa Viti Maalumu leo Mei 20, 2025, bungeni jijini Dodoma
Na Mwandishi Wetu - WHUSM

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema kuwa, Mfumo wa Artist Information Management System (AMIS) ambao umeunganishwa na TAUSI kutoka Ofisi ya Rais - TAMISEMI umerahisisha usajili wa Wasanii ambapo kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025 wasanii binafsi 844, vikundi 158, taasisi 39, kampuni 274 na kumbi za burudani 115 zimesajiliwa.

 

Mhe. Mwinjuma ameeleza hayo Mei 20, 2025, bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mhe. Lucy Sabu Mbunge wa Viti Maalumu kuhusu mikakati ya serikali kuhakikisha sekta ya sanaa na michezo inawanufaisha vijana kwa kuweka mifumo rasmi. 

 

Amesema, Serikali inaendelea kutoa mikopo ya masharti nafuu kwa wasanii kupitia Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ambapo, kiasi cha shilingi Bilioni 5. 25 zimetolewa kupitia benki ya CRDB na NBC kote nchini.

 

“Vilevile, Serikali imeanzisha tozo ya hakimiliki kwa lengo la kuwanufaisha wabunifu wakiwemo wasanii hususan vijana ambapo kati ya Septemba 2023 hadi Aprili 2025, jumla ya shilingi Bilioni 1.55 zimekusanywa”, amesema Mhe. Mwinjuma. 

 

Aidha, Mhe Mwinjuma ameeleza kuwa, mradi wa ujenzi wa Akademia ya Michezo katika Chuo cha Maendeleo ya michezo Malya nao unalenga kuibua vipaji hasa kwa vijana wenye umri mdogo, na ni miongoni mwa mikakati ya kuendeleza michezo. 

 

Ameongeza kuwa, mashindano ya UMISETA na UMITASHUMTA yanatumika kama njia ya kugundua na kukuza vipaji.

 

Akijibu swali la nyongeza la Mhe. Lucy Sabu kuhusu kukamilika kwa Akademia hiyo, Mhe. Mwinjuma amesema kuwa ujenzi huo utakamilika mwezi Desemba 2025.

 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi