Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Serikali Yatekeleza Mradi wa Kukabili Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar
May 20, 2025
Serikali Yatekeleza Mradi wa Kukabili Mabadiliko ya Tabianchi Zanzibar
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis akijibu maswali wakati wa Kikao cha 28 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 20 Mei, 2025.
Na Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)

 

 

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali inatekeleza mradi wa kuimarisha uwezo wa jamii za pwani kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika visiwa vya Unguja na Pemba wenye thamani ya Dola za Marekani milioni moja sawa na shilingi bilioni 2.7.

 

Amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na Mamlaka ya Usimamizi wa Mzingira Zanzibar (ZEMA).

 

Mhe. Khamis ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe.   Mohammed Jumah Soud aliyeuliza kwa nini NEMC haianzishi utaratibu wa kuishirikisha ZEMA ili kuongeza ufanisi wa uibuaji na usimamizi wa miradi ya mazingira Zanzibar wakati wa kipindi cha maswali na majibu leo Mei 20,2025 katika kikao cha 28 cha Mkutano wa 19 wa Bunge linaloendelea jijini Dodoma. 

 

Akiendelea kujibu swali hilo, Naibu Waziri Khamis alisema ili kuongeza ufanisi katika uhifadhi na usimamizi wa mazingira katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuna utaratibu wa ushirikiano kati ya NEMC na ZEMA katika uibuaji na usimamizi wa miradi ya mazingira.   

 

“Kuna miradi miwili inayoandaliwa kwa ushirikiano wa taasisi hizo mbili ikiwemo Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi katika maeneo yenye upungufu wa maji baridi ambao upo katika hatua za kupata kibali cha fedha kutoka Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (AF) na unatarajiwa kutekelezwa Unguja na Pemba kwa thamani ya Dola za Marekani milioni 3.5 (shilingi bilioni 9.5)”, amesema Mhe. Khamis.

 

Mhe. Khamis ameongeza kuwa, Mradi mwingine wa Kuimarisha Miundombinu katika Ukanda wa Pwani ili Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi upo katika hatua za kupitishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AFDB) na unatarajiwa kutekelezwa Tanzania Bara na Zanzibar. 

 

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Khamis amesema kupitia bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya mwaka 2025/26, Serikali inatarajia kutatua changamoto ya maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya wananchi.

 

Amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Nungwi, Mhe. Simai Hassan Sadiki aliyetaka kufahamu lini NEMC na ZEMA zitakuwa na ushirikiano ili kuondosha maji ya bahari yanayoathiri maeneo ya pwani ikiwemo Zanzibar.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi