Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amewataka Watanzania kuendelea kumtunza na kumuhifadhi nyuki ili kuwa na Taifa lenye uhakika wa chakula na uchumi ulio imara, kwa kuwa takribani asilimia 80 ya mimea ya chakula inayozalishwa duniani huchavushwa na nyuki.
Pia, Waziri Mkuu amezindua mpango kabambe utakaoleta mageuzi makubwa ya sekta ya ufugaji nyuki nchini unaojulikana kama Mpango wa Kuendeleza Sekta ya Ufugaji Nyuki kwa Tanzania Iliyo Bora (Achia Shoka, Kamata Mzinga).
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumanne, Mei 20, 2025) wakati akifunga Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani, ambayo kitaifa yamefanyika katika Kiwanja cha Chinangali jijini Dodoma. Ametoa wito kwa wadau wote wa masuala ya nyuki kushirikiana na Serikali kuwezesha utekelezaji wa mpango huo.
“Serikali inatumia maadhimisho kuhimiza, kuelimisha na kuhamasisha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zilizopo katika sekta hii, nyuki wana umuhimu mkubwa katika ustawi wa maisha ya binadamu, hususan katika uchavushaji wa mimea, uzalishaji wa chakula, uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.”
Waziri Mkuu amesema kupitia maadhimisho hayo, jamii hukumbushwa juu ya nafasi ya kipekee ya nyuki katika mnyororo wa maisha na umuhimu wa kuwalinda dhidi ya changamoto mbalimbali kama vile uharibifu wa mazingira, matumizi ya viuatilifu hatarishi, mabadiliko ya tabianchi na magonjwa.
Amesema Tanzania inazalisha tani 34,000 za asali na tani 1,918 za nta, kiwago ambacho kinaiweka nchi katika ramani ya dunia kwa kuwa ya kwanza kwa uzalishaji wa asali kwa nchi za Afrika Mashariki na SADC, nchi ya pili kwa Afrika na ya 14 duniani.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana amesema pamoja na kutambua umuhimu na mchango wa mdudu nyuki, maadhimisho hayo yanatoa nafasi kwa wananchi wa kutoka mikoa mbalimbali kujifunza na kutambua fursa zilizopo kwenye sekta hiyo ya ufugaji Nyuki.
Vilevile, Waziri huyo amesema wananchi wanapata nafasi ya kuelezwa mafanikio mbalimbali yaliyopatikana kwenye Sekta ya Ufugaji Nyuki katika kipindi hiki cha awamu ya sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia kuhusu mpango uliozinduliwa na Waziri Mkuu, Balozi Dkt. Pindi amesema mpango huo unalenga kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali kutoka tani 34,861 za sasa hadi kufikia tani 75,000 ifikapo Juni, 2035 na kuongeza mauzo ya mazao ya nyuki katika masoko ya kikanda na kimataifa. “Aidha, kupitia Mpango huo, takriban ajira mpya 43,055 zinatarajiwa kuzalishwa hasa kwa vijana na wanawake.”
Naye, Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda amesema amefurahishwa na mabadiliko makubwa yaliyofikiwa katika tasnia ya nyuki ikiwemo ubora wa asali na vifungashio, jambo ambalo limeiwezesha asali kutoka Tanzania kufanya vizuri kwenye masoko ya kimataifa na hivyo kuchangia kwenye kukuza uchumi.