Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Ummy: Hakuna Mgonjwa Aliyethibitishwa Kuwa na Ebola Nchini
Sep 14, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Eric Msuya – MAELEZO

Siku chache baada ya kutokea kwa Uvumi wa kuwepo kwa Ugonjwa wa Ebola Nchini, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia Waziri wake Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Wananchi wa Tanzania kutokuwa na hofu ya Ugonjwa huo kwani hakuna dalili wala Mgonjwa aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Mhe. Ummy Mwalimu amewahakikishia Wananchi, kuwa tangu kuripotiwa kwa Ugonjwa huo wa Ebola Nchi jirani, Serikali ya Tanzania imeweka mikakati mbalimbali ya kulinda Afya za Watanzania.

“Tumeimarisha utaratibu na ufuatiliaji wa Ugonjwa huu wa Ebola kupitia wataalamu wa Afya katika Mikoa, Wilaya na kuimarisha Uchunguzi wa Wageni wanaoingia Nchini kupitia mipaka yetu ya Tanzania” Alisema Mhe. Ummy Mwalimu

Sambamba na hilo Serikali kupitia Wizara ya Afya imenunua Vipima Joto  vya Mkono na Mavazi kinga (PPE) seti 2,670 na kusambaza katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Mwanza, Rukwa na Katavi kutokana na kuwepo kwa hatari ya kukumbwa na Ugonjwa huo.

Wizara ya  Afya inaendelea kuandaa mpango mkakati wa kutengeneza Kitini  na kutoa Elimu na  Mafunzo ya kukabiliana na Ugonjwa wa Ebola kupitia Waganga Wakuu wa Mikoa yote nchini pamoja na Watumishi 724 wa sekta ya Afya na Ngazi ya Jamii.

“Tumeanda Kitini chenye maelezo muhimu ya jinsi ya kukabiliana na Ugonjwa huu wa Ebola ikiwa sambamba na kutoa Elimu kupitia Vyombo vya Habari kwenye vitu mbalimbali kama vile Makala  fupi zinazotolewa na Waandishi wa Habari kwa kuandaliwa na Wizara ya Afya” Alisema Ummy Mwalimu

Aliongeza kuwa Wizara imetoa  Mafunzo juu ya kujikinga na Ugonjwa wa Ebola kwa Watumishi wa Afya zaidi ya 460 na  Ngazi ya Jamii zaidi ya 264, wakiwemo Viongozi wa Dini, Wanahabari, Vijana wa Bodaboda pamoja na Watendaji wa Vijiji walio katika Mikoa iliyo hatarini.

Serikali kupitia Wizara ya Afya imejenga uwezo na kununua Vifaa Tiba katika Maabara Kuu ya Taifa Jijini Dar es Salaam, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya pamoja na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa wa Tiba (KCRI) kilichopo katika Hospitali ya KCMC Mjini Moshi.

Waziri Ummy amewataka Wananchi kutopuuzia Dalili zozote zitakazo tokea kwenye Miili yao kwa kufika katika kituo cha Afya sababu Ugonjwa wa Ebola hauna tofauti na Dalili za Homa na Maralia

“Dalili kuu za ugonjwa wa Ebola ni Homa kali, kuumwa na kichwa, kutapika na kuharisha, viungo vya mwili kuuma, kutokwa na Vipele Mwilini na Damu katika Matundu ya Mwili” Alisema Ummy Mwalimu.

Wizara ya Afya imewataka Wanachi katika Mikoa yote Tanzania kujikinga  na kudhibiti Ugonjwa huu usiingie Nchini kwa kuepuka kugusa Damu, Mkojo, Jasho, Kinyesi, kunawa Mikono kupitia maji ya nayotiririka na kuepeuka Majimaji yanayotoka mwilini mwa mgonjwa mwenye Dalili za Ebola.

“Lakini pia tuna namba za simu Bure ambazo tumekuwa tukizisambaza  kwa Wananchi ambazo ni 0800110124 au 0800110125 hivyo wananchi watoa taarifa endapo akiziona dalili za ugonjwa wa Ebola” Alisema Ummy Mwalimu

Aidha, Waziri Ummy amewataka Wananchi wasidanganyike na kuepuka kusikiliza Habari za Uvumi wa Ugonjwa huo kutoka kwa Watu Mbalimbali wenyenia Ovu kwa Watanzania hivyo chombo pekee chenye kuweza kutoa taarifa za Magonjwa ya milipuko ni Wizara ya Afya.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Jamii Na. 1 ya Mwaka 2009, dhamana  ya kutoa Taarifa za Magonjwa ya milipuko ukiwemo huu wa Ebola ni Wizara  yenye dhamana na Masuala ya Afya, hivyo kwa sasa hakuna Ugonjwa wa Ebola Nchini.” Alisisitiza Ummy Mwalimu

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi