Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbas, amesema kuwa uzinduzi wa Uwanja wa Ndege wa Mtemere uliofanywa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba, katika Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, umeenda sambamba na uzinduzi wa miundombinu 21 ya utalii iliyojengwa katika Hifadhi za Taifa za Nyerere, Ruaha na Mikumi na Msitu wa Mazingira Asilia Kilombero.
Akizungumza leo Februari 11, 2026, wakati wa ukaribisho na utambulisho wa wageni mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa uwanja huo, Dkt. Abbas amesema kuanza kutumika kwa miundombinu hiyo ni hatua ya kihistoria katika maendeleo na ustawi wa sekta ya uhifadhi na utalii nchini.

Amesema miradi hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuboresha huduma za utalii, kuongeza ushindani wa vivutio vya Tanzania kimataifa na kuimarisha usimamizi endelevu wa rasilimali za maliasili.
Kwa mujibu wa Dkt. Abbas, ujenzi wa miundombinu hiyo umeongeza ubora wa vivutio vya utalii katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, eneo ambalo linaendelea kukua kwa kasi katika kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi. Aidha, hatua hiyo itaongeza ufanisi wa usimamizi wa hifadhi na kuboresha huduma kwa wageni.

“Miundombinu hii itafungua fursa mpya za kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hizi, hususan kupitia ongezeko la shughuli za utalii zitakazochochea ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja,” amesema Dkt. Abbas.
Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wa sekta ya uhifadhi na utalii, ambao wameendelea kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha miundombinu na kukuza sekta hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.
Uzinduzi wa miradi hiyo unaashiria dhamira ya Serikali ya kuendeleza utalii kwa njia endelevu, sambamba na kulinda na kuhifadhi rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.