[caption id="attachment_41066" align="aligncenter" width="750"] Mheshimiwa Waziri, Ummy Mwalimu (katikati), akiongoza Mkutano na Wadau wa Kemikali uliokuwa na lengo la kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya kemikali nchini. kulia ni Mwenyekiti wa Bodi Tendaji ya Mamlaka, Profesa Esther Hellen Jason na Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (kushoto).[/caption]
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali itaendelea kusimamia na kudhibiti matumizi ya kemikali ili kuhakikisha hazileti madhara kwa afya za wananchi na Mazingira.
Waziri Ummy ameyazungumza hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano na wadau wanaojishughulisha na shughuli za kemikali ulioandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara ya kemikali nchini.
“Kemikali zisipodhibitiwa vizuri zinaweza kuleta madhara katika afya, mazingira pamoja na kuhatarisha usalama wa nchi, ipo haja ya kuweka mazingira mazuri ya kusimamia na kudhibiti uingizaji na matumizi ya kemikali nchini ili zisilete madhara,” alisema Ummy.
[caption id="attachment_41065" align="aligncenter" width="750"] Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko (kushoto) akifafanua jambo kwa Mheshimiwa Ummy Mwalimu, wakati wa Mkutano na Wadau leo.[/caption]Alifafanua kuwa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2014 zinaonyesha vifo milioni 12.6 vilitokana na mazingira duni ya kuishi, mojawapo ya kichocheo ni athari za kemikali ambazo zimekuwa zikisababisha magonjwa na vifo.”
Waziri Ummy aliongeza kuwa kemikali zimekuwa na athari kubwa kwa binadamu kwa kusababisha magonjwa zaidi ya mia moja yakiwemo magonjwa ya moyo, saratani, ngozi, athari katika mifumo ya fahamu, upumaji pamoja na chakula kuathiri zaidi wananchi wengi.
“Tukubali kuwa kemikali zina madhara kwa wananchi lakini sasa tuwe na mazingira mazuri ya kuzidhibiti, Serikali itaendelea kuboresha mazingira mazuri kwa wafanya biashara ya kemikali nchini,” Ummy aliongeza.
Aidha, Waziri Ummy amezitaka Taasisi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA) pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA) kuangalia upya tozo zinazotozwa kwa wafanyabiashara wa kemikali nchini pamoja na kupunguza changamoto zisizo za lazima ili kuwawekea mazingira rafiki wafanya biashara za kemikali.
Amezitaka Taasisi hizo kutokuwa na vikwazo kwa uwekezaji na biashara, kikwazo cha kushamiri na kukua kwa uwekezaji nchini na badala yake wawe mawakala wa kukuza biashara na uchumi nchini ili kuvutia wawekezaji kwa kuweka mazingira rafiki kwa biashara.
[caption id="attachment_41067" align="aligncenter" width="750"] Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Mhandisi Anthony Swai akichangia mada[/caption] [caption id="attachment_41069" align="aligncenter" width="750"] Mfanyabiashara Bw. Azim Dewji akichangia mada wakati wa Mkutano.[/caption] [caption id="attachment_41068" align="aligncenter" width="750"] Menejimenti na baadhi ya watumishi wa Mamlaka wakifuatilia uchangiaji mada uliokuwa unawasilishwa na wadau mbalimbali walioshiriki Mkutano huo.[/caption]Awali akisoma taarifa yake Mkemia Mkuu wa Serikali Dkt. Fidelice Mafumiko, amesema Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Namba. 3 ya mwaka 2003 imekuwa na mchango mkubwa katika udhibiti wa matumizi ya kemikali nchini.
“Kabla ya kutungwa kwa sheria hii, kemikali zilikuwa zikiingizwa nchini kiholela na kutumika bila ya kuwa na ufuatiliaji au udhibiti wowote ila baada ya kutungwa kwa Sheria hii imewezesha kudhibiti usafirishaji, utumiaji pamoja uteketezaji wa taka zinazotokana na kemikali,” alisema Dkt. Mafumiko.
Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) Mhandisi Anthony Swai, amesema tozo zimekuwa nyingi kiasi cha kuwaumiza wafanyabiashara huku akiiomba Serikali kuainisha mipaka ya taasisi za umma pamoja na tozo wanazostahili kulipa kwani kumekuwa na mwingiliano wa majukumu baina ya taasisi kama TFDA na TBS.
[caption id="attachment_41063" align="aligncenter" width="1000"] Mgeni Rasmi na Mwenyekiti wa Mkutano, Mhe. Ummy Mwalimu (aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wajumbe wa Bodi Tendaji ya Mamlaka wakiwa pamoja na baadhi ya wadau walioshiriki Mkutano (picha ya juu).[/caption]