[caption id="attachment_11836" align="aligncenter" width="750"] Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya ziara yake nchini India katika mkutano wa pamoja wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili, kulia ni Kaimu Mkurugenzi Idara ya Uwekezaji Aristides Mbwasi.[/caption]
Na. Paschal Dotto.
Watanzania wametakiwa kuwekeza zaidi katika viwanda vidogovidogo ili kuinua uchumi na kujenga Tanzania ya viwanda kwakuwa uanzishaji wa viwanda vidogo hauhitaji uwekezaji mkubwa.
Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage,alipokuwa akitoa mrejesho wa ziara aliyoifanya nchini India katika mkutano wa 4 wa pamoja katika masuala ya biashara ulitokana na makubaliano ya January 14, 2002 baada ya Tanzania na India kusaini mkataba wa ushirikaiano katika masuala ya viwanda na biashara.
[caption id="attachment_11837" align="aligncenter" width="750"] Waandishi wa habari wakimsikiliza Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage (kushoto) wakati akitoa taarifa ya ziara yake nchini India katika mkutano wa pamoja wa kibiashara baina ya nchi hizi mbili. Picha na Eliphace Marwa.[/caption]Alisema baadhi ya mambo yalijadiliwa katika mkutano huu ni pamoaja na mkataba wa kuhamasisha na kulinda uwekezaji kwakuwa India ni moja ya nchi tano kubwa zilizowekeza nchini Tanzania hususani katika viwanda vya kuzalisha bidhaa.
“Hakuna nchi nzuri ya kuwekeza kama Tanzania kwa sababu Tanzania haitaifishi mali za wawekezaji nasema hili ili wawekezaji wajue na waondoe wasiwasi ”, alisema Waziri Mwijage.
Maeneo mengine ambayo yalipewa kipaumbele katika mkutano huo ni pamoja ushirikiano katika usimamizi wa Forodha, ambapo India iko pamoja na Tanzania katika kuhakikisha inaepusha udanganyifu wa bidhaa zinazo agizwa na wafanyabiashara wakubwa nchini.
“Viwanda vyetu vimekufa kwa sababu wafanyabiashara wetu wanatoa taarifa za uongo kuhusu bidhaa walizo nunua nje na kuingiza nchini kwa hiyo bidhaa zetu zinashindwa kuhimili ushindani kwa kushuka kwa bei zilizoagizwa”, alisisitiza Waziri Mwijage.
Akizungumzia kuhusu viwanda vidogo vidogo Waziri Mwijage alisema SIDO ni mwalimu kwa nchi nzima kwa sababu wapo mikoa yote Tanzania na ndiyo itakuwa kiongozi katika suala la ujenzi wa viwanda vidogovidogo nchini.
Utaalam ambao wawakilishi wa SIDO wameupata kutoka India pamoja na mbia aliyekubali kuingia nao mkataba utawasaidia sana kujenga henga kubwa la viwanda vidogovidogo kwa ajili ya kutoa elimu kwa Watanzania wote.
Kwa upande wa utafiti katika masuala ya uchumi na viwanda kampuni ya utafiti (TIRDO) iliyoambatana na Waziri Mwijage imeingia mkataba na kampuni ya utafiti ya nchini India (CSIR) na kupata ujuzi katika masuala ya ukamuaji wa mbegu za mwarobaini kwaajili ya kupata kemikali za kuua wadudu.
Waziri Mwijage alisema mfano wa viwanda vidogo ambavyo vinaweza kuwakomboa watanzania ni pamoja na mitambo midogo ya kutengeza saruji, mashine ndogo za ujenzi, matrekta madogo kwa kilimo cha kawaida, viwanda vya kutengeneza Korosho, viwanda vya kuchakata ngozi na kutengeneza viatu pamoja na mashine za kusaga unga.
Serikali ya India imeendelea kwani asilimia 38 ya maendeleo yake yanatokana na viwanda vidogovidogo kwa hiyo Tanzania tunatakiwa kuwekeza zaidi katika viwanda hivyo ili kupata pato kubwa, kuongeza ajira na hatimaye kukuza uchumi.
Waziri Mwijage alisema katika nchi ya India asilimia 42 hadi 45 ya bidhaa zinazouzwa nje zinazalishwa katika viwanda vidogovidogo, hivyo hata sisi tunaweza kupunguza uingizaji wa bidhaa kutoka nje kwani kwa sasa zaidi ya shilingi trioni 2 zinatumika kuagiza bidhaa ndogondogo kama maziwa na juice kitu kinachowezekana kutengenezwa hapa nchini.