Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) ameshiriki Mkutano wa 1,094 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 27 Julai, 2022.
Mkutano huo ulilenga kupokea na kujadili taarifa ya Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu hali ya amani na usalama ya nchini Somalia na shughuli za Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (The African Union Transition Mission in Somalia –ATMIS).
Taarifa hiyo ambayo iliyowasilishwa na Mhe. Mahmoud Ali Youssouf, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Jamhuri ya Djibouti ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama kwa mwezi Julai 2022, pamoja na mambo mengine iliangazia masuala yafuatayo; Hali ya kisiasa ya nchini Somalia na kukamilika kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu (political Development and update on National Elections), Hali ya Usalama na Maendeleo ya Shughuli za Pamoja katika Kusaidia Mpango wa Mpito wa Somalia na Usanifu wa Usalama wa Kitaifa.
Masuala mengine ni kuangazia hali ya Maendeleo katika utekelezaji wa Pendekezo la Pamoja na Dhana ya Uendeshaji, Masuala yanayohusiana na kuimarisha Hali ya Kibinadamu nchini Somalia na Ufadhili endelevu wa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia
Akichangia katika mkutano huo, Waziri Mulamula alianza kwa kumpongeza Mhe. Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Serikali ya Shirikisho la Somalia. Vilevile alitumia nafasi hiyo kuelezea matumaini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa nchi hiyo baada ya kukamilisha vyema zoezi la uchaguzi sasa kunawapa fursa na hali mpya ya kuweka nguvu katika kutekeleza mambo muhimu kama yalivyoainishwa katika Mpango wa Mpito wa Somalia, kama vile kujenga taasisi za serikali, na kuongeza nguvu katika maandalizi ya makabidhiano ya serikali kwa amani na usalama.
Aidha, Waziri Mulamula alitoa wito kwa Kikosi cha Mpito cha Umoja wa Afrika nchini Somalia (ATMIS), Umoja wa Mataifa na Serikali ya Shirikisho la Somalia kufanya kazi kwa pamoja katika kushughulikia masuala muhimu yatakayo leta amani ya kudumu sambamba na kutazama suala la vikwazo vya silaha dhidi vilivyowekwa dhidi ya Somalia.
Mkutano huo umetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuzingatia kwa haraka maombi ya Serikali ya Shirikisho la Somalia kuhusu kuondolewa vikwazo vya silaha vilivyowekwa dhidi ya nchi yao, ili kuiongezea nchi hiyo uwezo wa kutosha wa kukabiliana vilivyo na tishio la usalama linaloletwa na kundi la kigaidi la Al Shabaab.
Vilevile, mkutano uliipongeza Serikali ya Shirikisho la Somalia kwa kumchagua Naibu Spika mwanamke wa kwanza katika historia ya nchi hiyo. Pia ulisisitiza kuhusu umuhimu wa Serikali ya Somalia kuendelea kutambua nafasi ya wanawake, vijana, mashirika ya kiraia pamoja na vyombo vya habari katika mchakato wa mpito ambao utaifanya Somalia kufikia lengo la asilimia 30 kama ilivyokubaliwa katika Makubaliano ya Uchaguzi wa tarehe 17 Septemba 2020 na 27 Mei, 2021.
Tanzania ni miongoni mwa wajumbe 15 wa Baraza hilo. Wajumbe wengine ni Burundi, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Gambia, Ghana, Morocco, Namibia, Nigeria, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia, Uganda na Zimbabwe.