Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa Bashay, wilayani Karatu watumie fursa zinazojitokeza kwenye sekta ya utalii kuboresha maisha yao.
“Tumieni fursa ya uwepo wa eneo hili. Halmashauri wakishajenga vizimba vya biashara, leteni bidhaa zenu kama vile picha za tingatinga, mapambo, vinyago na vyakula vya asili ili watalii wakija hapa wapate huduma kutoka kwenu,” alisema.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Julai 21, 2019) wakati akizindua mradi wa ujenzi wa vituo vya polisi vya kupunguza changamoto kwa magari ya utalii barabarani na kukabidhi gari la polisi kwa ajili ya patrol ya watalii katika eneo la Bashay, wilayani Karatu, mkoani Arusha.
Waziri Mkuu alizindua kituo cha kutolea huduma za usalama kwa watalii wilayani Karatu ikiwa ni ishara ya kuwakilisha vituo vingine vitatu vinavyoendelea kujengwa mkoani Arusha katika maeneo ya Kikatiti (Arumeru), Makuyuni (Monduli) na Engikaret (Longido).
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwasihi wakazi hao wawalinde watalii ili waitangaze vema nchi ya Tanzania pindi wakirudi makwao. “Ili kukuza na kutangaza utalii, tunapaswa tuwe na mapenzi mema kwa watalii lakini kikubwa zaidi ni usalama wao.”
Aliwataka wakazi hao waendelee kuiamini Serikali ya awamu ya tano na waendelee kumuombea Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili apate nguvu ya kuleta maendeleo zaidi.
Pia aliwashukuru viongozi wa Tanzania Association of Tour Operators (TATO) kwa kuchangia ujenzi wa vituo hivyo na kutoa gari jipya la polisi kwa ajili kituo hicho cha Karatu. Gari hilo aina ya Toyota Landcruiser lililogharimu dola za Marekani 45,000, limepewa namba za usajili za PT 4190.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wakazi wa Bashay waliohudhuria hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo alisema ujenzi wa vituo hivyo umetokana na malalamiko aliyopokea kwamba watalii wakitoka uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) hadi kufika Karatu wanakuwa wamesimamishwa njiani zaidi ya mara 20.
“Tulijiuliza hawa watalii wamekuja kutalii, wanataka kupumzika, sasa ni kwa nini wasumbuliwe kiasi hicho? Tuliamua kuanzisha vituo vya aina hii, ili watalii wafanyiwe ukaguzi kwenye check-points maalum,” alisema.
Aliomba Jeshi la Polisi liwapange barabarani askari ambao ni weledi na wana uelewa wa masuala ya utalii na kutolea mfano wa wiki iliyopita ambapo alikuwa akitokea mjini kwenda Karatu na kukuta magari ya watalii zaidi ya 10 yamesimamishwa njiani.
“Niliona baadhi yao wakiwa wamelala kwenye magari kwa uchovu, nilipowauliza wamekalishwa kwa muda gani, walisema ni kwa zaidi ya dakika 45. Nilipomuuliza askari aliyewasimamisha ni kwa nini anafanya hivyo, akanijibu kwamba dereva amemjibu vibaya. Hivi ni kwa nini watalii wateseke juani wakati mwenye makosa ni dreva?”
Naye, Makamu Mwenyekiti wa TATO, Bw. Henry Kimaro aliishukuru Serikali kwa jitihada inazofanya za kupambana na ujangili na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini. “Tumeona hivi karibuni watalii wengine kutoka Israel, China na sasa ndege yetu imeanza kwenda India kuwafuata hukohuko,” alisema.
Alisema wameanza na vituo hivyo vinne mkoani Arusha lakini tatizo hilo liko maeneo mengi nchini na wao hawawezi kufika nchi nzima kutoa huduma kama hiyo. Hivyo, alimuomba Waziri Mkuu awahimize Wakuu wa Wilaya ambao wilaya zao zinajihusisha na sekta ya utalii, waige mfano wa wilaya ya Karatu ili kuhakikisha usalama wa watalii wawapo nchini.