Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezionya Halmashauri za Wilaya na Manispaa zilizoshindwa kufikisha malengo ya makusanyo ya kodi na kuzitaka zijitathmini ni kwa nini hazijafikisha malengo hayo.
“Kuna Halmashauri zimetajwa hapa kwamba hazijafikisha malengo ya makusanyo ya ndani. Fanyeni tathmini, ni kwa nini hamjafikia malengo na mhakikishe kuwa mwakani hamji kutajwa tena kwenye mkutano kama huu,” alisema. Halmashauri hizo ni Kakonko, Buhigwe, Madaba, Kigoma, Momba na Songea.
Ametoa agizo hilo leo mchana (Jumanne, Julai 23, 2019) wakati akizungumza na washiriki wapatao 700 ambao ni wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa (ALAT) unaoendelea jijini Mwanza.
Waziri Mkuu ambaye amefungua mkutano huo wa siku tatu kwa niaba ya Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, amewataka washiriki wa mkutano ambao ni Mameya, Wenyeviti wa Halmashauri, Wakurugenzi wa Majiji, Miji na Manispaa, wasimamie makusanyo ya mapato kupitia vyanzo vyao ili waweze kupanga mipango ya maendeleo. “Lengo la Serikali ni kuwezesha kila Halmashauri zijitegemee kwa asilimia 80-100 ifikapo 2025,” amesema.
“Katika makusanyo hayo, hakikisheni kuwa mnatenga asilimia 40 kwa ajili ya shughuli za maendeleo. Na hili ni tatizo kwa Halmashauri nyingi zikiwemo zile kubwa. Ukifuatilia kwa makini huoni miradi inayogusa maisha ya wananchi wa kawaida.”
“Ukichukulia Dar es Salaam au Arusha ambao wanakusanya kati ya shilingi bilioni tano na 10, ni mradi gani wa thamani kubwa uliojengwa kwa kutumia fedha zenu za ndani, ukiacha hii mikubwa ya stendi za mabasi au barabara za lami ambayo inajengwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu?” alihoji.
“Hivi kuna Halmashauri ambayo imejenga kituo cha afya cha kisasa kwa kutumia fedha zake za makusanyo? Afadhali hawa wa Dodoma ambao wameanza kujenga stendi ya mabasi na hoteli mbili za kitega uchumi,” amesema.
“Uamuzi wa Mheshimiwa Rais Magufuli wa kukusanya fedha zote na kuziweka kwenye chanzo kimoja ulitokana na study ya muda mrefu iliyofanyika na kubaini kuwa fedha zinazokusanywa haziendi kwenye miradi inayogusa wananchi. Niwasihi sana, fanyeni miradi ambayo kila Mtanzania angependa kuiona kwenye Mamlaka zenu za Serikali za Mitaa,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba Serikali iliamua kumuondoa aliyekuwa Katibu Mkuu wa ALAT, Bw. Abraham Shamumoyo kwa sababu ya utendaji mbovu.
“Kuna maamuzi alikuwa akiyafanya bila kuishirikisha Kamatai ya Utendaji. Kuna mikataba ilikuwa ikifanyika na mingine inahusisha hadi mataifa ya nje. Kuna fedha zilitolewa, zikawekwa kwenye akaunti binafsi na siyo akaunti ya ALAT,” amesema.
Amesema ALAT ni taasisi kubwa ya Serikali ambayo inahitaji kuheshimiwa, na siyo ya kuancha iendeshwe na mtu mmoja kama atakavyo. “ALAT ni taasisi kubwana Serikali inaitegemea. Niwahakikishie kuwa Mheshimiwa Rais, anawathamini, anawapenda na anataka mchape kazi kuisaidia Serikali yenu,” amesema.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na washiriki wa mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, Bw. Suleiman Jafo alisema Serikali inajivunia ujenzi wa shule za sekondari za kata ambazo mwaka huu zimefanya vizuri kwenye mitihani ya kuhitimu kidato cha sita.
“Kati ya shule bora 100, shule 64 ni za Serikali na kazi ya shule hizo 64, shule 54 ni za kata. Na kwenye matokeo ya masomo ya sanaa, kati wanafuzi bora 10 wa kiume, wanafunzi saba wanatoka kwenye shule za kata,” alisema.
Alisema Serikali ya awamu ya tano imewekeza sana kwenye sekta ya elimu, ikiwemo ujenzi wa shule za sekondari na ukarabati wa shule kongwe za sekondari.
Alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa kutenga sh. bilioni 268.8 kwa ajili ya ujenzi wa miradi 38 ya kimkakati kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vile ujenzi wa masoko, machinjio na stendi za mabasi.