16 SEPTEMBA , 2017
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua miongozo ya Kitaifa ya Kusimamia Mafunzo ya Vitendo kwa Wahitimu (Internship Guidelines) na Mafunzo ya Uanagenzi (Apprenticeship Guidelines) mahala pa kazi, leo (Jumamosi, Septemba 16) mjini Dodoma.
Amesema miongozo hiyo inalenga kuongeza ari kwa waajiri na wadau wengine kushiriki katika kutoa mafunzo ya kukuza ujuzi na stadi za kazi ili kuhakikisha wahitimu na wanagenzi wanapata stadi za kazi na ujuzi stahiki wa kuajirika au kujiajiri.
Waziri Mkuu amesema miongozo hiyo ambayo inakwenda kuboresha mafunzo ya uanagenzi na kwa wahitimu itachochea ukuzaji wa viwanda na kupunguza ukosefu wa ajira kwa watanzania hususan vijana.
Amesema Serikali imekua ikipokea malalamiko kutoka kwa waajiri kwamba wahitimu wengi wa ngazi mbalimbali za mafunzo wanaingia katika soko la ajira wakiwa hawana ujuzi unaohitajika na hivyo waajiri kulazimika kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Amesema baada ya kupokea malalamiko hayo Serikali, Waajiri na Wafanyakazi na walikubaliana kuimarisha mfumo wa utoaji mafunzo yanayofanyika maeneo ya kazi ili kuhakikisha mafunzo yatolewayo maeneo ya kazi yana ubora unaohitajika.
“Kuimarisha uwezo wa nguvu kazi ya Taifa ni muhimu na njia bora ni kuboresha utoaji mafunzo kwa vitendo mahali pa kazi kwa kuweka miongozo bora itakayowaongoza wadau wote wakiwemo Serikali, Waajiri, Wafanyakazi na Vijana kutoa Mafunzo.”
Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. John Magufuli alipoanza kuweka malengo ya ujenzi wa viwanda, mbali na kuwezesha kukua kwa kilimo na kuongeza thamani mazao, pia alilenga kupanua wigo wa ajira za viwandani ambapo kiwanda kinaweza kuajiri watu zaidi ya 1000.
Amesema miongozo hiyo itasaidia kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuhakikisha Taifa linakuwa na nguvu kazi yenye weledi wa kutosheleza mahitaji ya soko la ajira na kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama amesema miongozo hiyo inaweka mfumo madhubuti wa kuandaa, kutekeleza, kusimamia, kuratibu na kufuatilia mafunzo husika mahala pa kazi.
Pia miongozo hiyo inabainisha majukumu ya wadau muhimu wa mafunzo hayo ambayo ni pamoja na kuweka bayana utaratibu wa kugharamia mafunzo ikiwa ni pamoja na kushirikisha Serikali, waajiri na wazazi.
“Miongozo imebainisha majukumu ya wadau katika kutoa mafunzo ambao ni Serikali, waajiri, taasisi za mafunzo, taasisi za mitaala na wanagenzi na wahitimu. Pia imebainisha vigezo vya kuwapata washiriki wa mafunzo na muda wa mafunzo.”
Pia miongozo hiyo imebainisha mfumo wa kitaasisi wa kuratibu na kuhakikisha ubora wa mafunzo kwa kuunda kamati ya Utatu wa Taifa ya kuratibu, kufuatilia tathmini ya mafunzo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
40480 - DODOMA.
JUMAMOSI, SEPTEMBA 16, 2017