[caption id="attachment_13625" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa akikata keki ikiwa ni ishara ya Maadhimisho ya miaka 40 ya Kituo cha AMGC tangu kuanzishwa kwake. Wanaoshuhudia kutoka kushoto Mwenyekiti wa AUC, Frank Mugenyi, Mkurugenzi Mkuu Kituo cha AMGC, Ibrahim Shaddad na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani (kulia).[/caption]
Na: Asteria Muhozya na Rhoda James - MEM
Wanachama wa Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC), wametakiwa kuweka mazingira rafiki kuvutia uwekezaji kwenye eneo la uendelezaji Madini ikiwemo kuandaa Rasilimali Watu, Maarifa na vitendea kazi ili kuwezesha usimamizi mzuri wa Sekta ya Madini utakaowezesha tija kwa nchi husika.
Hayo yamesemwa leo na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa wakati akifungua Mkutano wa 37 Baraza la Uongozi wa Kituo cha Madini na Kijiosayansi cha Afrika (AMGC) kilichopo Kunduchi jijini Dar es Salaam.
[caption id="attachment_13626" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (katikati) akielekea kuaangalia maabara mbalimbali katika kituo cha AMGC. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu kituo cha AMGC, Ibrahim Shaddad na kulia ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani. Wengine ni washiriki wa mkutano huo.[/caption]Waziri Mkuu amesema kuwa, bado kituo cha AMGC hakijatumika vema kwa mujibu wa kusudio la uanzishwaji wake na endapo kikitumiwa vizuri kinaweza kutoa tija kwenye sekta ya uchimbaji madini, uongezaji wa thamani na usimamizi wa sekta hiyo ikiwemo masuala ya usimamizi wa mazingira yanayozingatiwa.
“Nawakumbusha ndugu wajumbe na wanachama wa AMGC kuwa kituo hiki bado hakijatumika ipasavyo. Ni vema tukitumie ili kupata tija kwenye uendelezaji na usimamizi wa madini yetu.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, zaidi ya miongo minne iliyopita waasisi wa mataifa wa nchi wanachama walifikiria wazo la kuwa na Kituo cha kuweza kujenga uwezo wa wataalamu wa kusimamia sekta ya madini ambapo moja ya vituo hivyo ni kituo cha AMGC ambapo leo tarehe 14 Septemba, 2017, kimetimiza miaka 40 tangu kuanzishwa kwake.
[caption id="attachment_13627" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ( katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa kituo cha AMGC.[/caption]Ameeleza kuwa, AMGC ni moja ya Taasisi chache za aina yake Duniani chenye teknolojia za kisasa ambazo zinaweza kusaidia kufanya uchambuzi wa miamba na madini.
Pia, ameongeza kuwa, kituo hicho ni sehemu ambayo inasaidia kupata huduma za ushauri wa kiteknolojia zinazoweza kutumika kufanya uzalishaji wa madini mbalimbali.
Ameeleza kuwa taarifa za Kiojiolojia zinaonesha kuwa, Afrika ni Bara lenye utajiri mkubwa wa rasilimali madini ikiwemo nchi wanachama wa AMGC na kwamba, sehemu kubwa ya madini hayo hayajaanza kutumika au yako katika hatua mbalimbali za uendelezaji.
[caption id="attachment_13628" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mtaalam Mshauri wa kituo cha AMGC, Timo Gawronski kuhusu namna Maabara ya Kisasa ya Upimaji Madini ambayo inaonesha asili ya madini ya mahali yaliyochimbwa.[/caption]Aidha, ametoa mfano wa Nchi ya Tanzania kuwa, licha ya kuwa na madini ya Almasi, Shaba, Chuma na madini ya vito kama Tanzanite na mengineyo, lakini mchango wa sekta husika ni asilimia 4.8 ya pato la Taifa.
Aidha, amewataka nchi wanachama kuzifanyia kazi changamoto zinazokikabili kituo hicho ikiwemo kulipa ada za uanachama, kukiletea wateja kituo ili kiweze kutimiza malengo yake na kukifanya kutoa huduma bora zaidi ya zinazotolewa sasa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani akizungumza katika Mkutano huo, amesema kuwa moja ya mikakati ya nchi wanachama ni kukifanya kituo hicho kuanza kufanya shughuli za uchenjuaji madini kutokana pia na mahitaji ya huduma hiyo kwa Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Aidha, ameongeza kuwa, mikakati mingine ya nchi wanachama ni kukifanya kituo hicho kijulikane duniani ikiwemo kukifanya kuwa bora zaidi.
Katika hatua nyingine, nchi wanachama wa AMGC wameichagua Tanzania kuendelea kuwa Mwenyekiti wa kituo hicho kutokana na msimamo wa Serikali katika udhibiti wa rasilimali madini ambao umeoneshwa na Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Kituo cha AMGC kilianzishwa mwaka 1977, lengo likiwa ni kuhakikisha Sekta ya Madini inawajibika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi pia ikijali masuala ya mazingira.
Kituo hiki kinafundisha wataalamu na, kufanya tafiti na pia kina maabara ya kisasa kwa ajili ya uhakiki na uongezaji thamani wa madini.