Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Apokea Ripoti za Uchunguzi wa Biashara ya Almasi na Tanzanite
Sep 06, 2017
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_12313" align="aligncenter" width="750"] Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai Taarifa ya Kamati Maalum ya Bunge ya Kuchunguza Biashara ya Tanzanite na Almasi kwenye viwanja vya Bunge mjini Dodoma Septemba 6, 2017. Katikati ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe.[/caption]

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea ripoti mbili za kamati ya Maalumu ya Bunge ya kuchunguza biashara ya madini ya almasi na tanzanite na kuahidi kuiwasilisha kwa Rais Dkt. John Magufuli kesho asubuhi.

Pia amesema Serikali haina mchezo katika usimamizi wa rasilimali za Taifa, hivyo amewataka viongozi  na watendaji wote waliokabidhiwa dhamana ya kusimamia sekta ya madini hakikisha wanatimiza vyema wajibu wao.

Waziri Mkuu amepokea ripoti hizo leo (Jumatano, Septemba 6, 2017) kutoka kwa Spika wa Bunge, Bw. Job Ndugai ambaye alikabidhiwa ripoti hizo  na Wenyeviti wa kamati Bw. Mussa Zungu (Almasi) na Bw. Dotto Biteko (Tanzanite).

“Kesho saa 4.30 asubihi nitaziwasilisha ripoti hizi kwa Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli. Hakuna ucheleweshaji katika jambo hili na Mheshimiwa Spika (Job Ndugai) kesho twende tukakabidhi wote.”

Waziri Mkuu amesema kamati hizo zimefanya kazi nzuri na kwamba Serikali inaimani  na ripoti hizo na ushauri uliotolewa utawezesha Taifa kunufaika na rasilimali zake, hivyo mapendekezo na hoja zote zilizoibuliwa zitafanyiwa kazi katika kipindi kifupi.

Amesema taarifa hiyo zimewasilishwa katika kipindi muafaka na zimeonyesha  dhamira ya dhati ya Bunge, kuunga  mkono juhudi za Rais Dkt. Magufuli  na Serikali yote kwa ujumla katika kulinda rasilimali za Taifa.

“Watanzania ni mashahidi kwamba Mwenyezi Mungu ameijalia Tanzania utajiri wa rasilimali za kila aina.  Tunayo ardhi yenye rutuba, madini ya aina mbalimbali na mengine hayapatikani katika nchi nyingine isipokuwa Tanzania tu kama vile Tanzanite.”

Amesema ni  lazima rasilimali hizo zisimamiwe na kutunzwa vizuri ili ziwezeshe kuboresha hali na maisha ya Watanzania wote na kila mwananchi ana jukumu la kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi katika Sekta ya madini nchini.

Waziri Mkuu amesema suala la kusimamia rasirimali za nchi ni la Watanzania wote kama ilivyoainishwa kwenye ibara ya 27 ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ambapo aliinukuu Ibara hiyo kama ifuatavyo:

“27 (1) kila mtu ana wajibu wa kulinda mali asilia ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mali ya Mamlaka ya Nchi na mali yote inayomilikiwa kwa pamoja na Wananchi na pia kuiheshimu mali ya mtu mwingine.

“(2) Watu wote watatakiwa na Sheria kutunza vizuri mali ya Mamlaka ya nchi na pamoja vita aina zote za uharibifu na ubadhilifu na kuendesha uchumi wa Taifa na kuendesha uchumi wa taifa kwa makini kama watu ambao ndio waamuzi wa hali ya baadaye ya taifa lao.”

Kamati hizo zilipewa jukumu la kutathmini mfumo wa uchimbaji, usimamizi, umiliki na udhibiti wa madini ya Tanzanite na Almasi Nchini, ambazo zimeishauri Serikali kuhusiana na mfumo bora wa uendeshaji na udhibiti wa biashara ya Tanzanite na Almasi  nchini.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S.L.P 980,

40480-DODOMA 

JUMATANO, SEPTEMBA 6, 2017.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi