Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Apokea Msaada wa Vyerehani
Sep 08, 2017
Na Msemaji Mkuu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea msaada wa vyerehani 25 kutoka katika Taasisi ya African Releaf Organization ya nchini Kuwait.

Amepokea msaada huo  leo (Ijumaa, Septemba 9, 2017) kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wananchi wa jimbo la Ruangwa.

Waziri Mkuu ameishukuru taasisi hiyo kwa msaada huo wa vyerehani ambavyo vitagawiwa kwenye vikundi mbalimbali vya wajasiriamali wilayani Ruangwa.

Amesema vyerehani hivyo vitawawezesha wajasiriamali wanaojishughulisha na ushonaji kupata vitendeakazi vitakavyotumika kama njia ya kujiongezea kipato.

Waziri Mkuu amesema mbali na kutoa msaada huo wa vyerehani pia taasisi hiyo inajenga Zahanati katika kijiji cha Mbecha kata ya Nanganga wilayani Ruangwa.

“Taasisi hii ni rafiki na Halmashauri yetu na Wanaruangwa wamefarijika kwa kupata zahanati na  vyerehani vitakavyotumika kama njia ya kujiongezea kipato.”

Awali, Mkurugenzi wa Miradi wa Taasisi ya African Releaf Organization, Bw. Khamis Mkanachi alishukuru kwa ushirikiano wanaoupa kutoka Halmashauri ya Ruangwa.

Pia Bw. Mkanachi amesema taasisi yao itaendelea kuvisaidia vikundi mbalimbali vya ujasiriamali katika Halmashauri hiyo kwa lengo la kuvikwamua kiuchumi.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu alimtembelea na kumpa pole mbunge wa jimbo la Newala Vijijini, Bw. Rashidi Akbar aliyelazwa katika Taasisi Moyo ya Jakaya Kikwete.

Kwa upande wake Bw. Akbar alimshukuru Waziri Mkuu kwa kumtembelea hospitalini hapo na kwamba hali yake kwa sasa inaendelea vizuri ukilinganisha na alivyofikishwa.

Pia Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kumjulia hali Bw. Anzigar Kambanga ambaye ni mwananchi wa wilaya ya Ruangwa aliyelazwa katika Taasisi Moyo ya Jakaya Kikwete.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

IJUMAA, SEPTEMBA 9, 2017.

       

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi