Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amefunga soko la wakimbizi na wananchi lililoanzishwa nje ya kambi ya Nduta iliyopo wilayani Kibondo mkoani Kigoma.
Hatua hiyo imekuja baada ya soko hilo kubainika kuwa chanzo cha wakimbizi kutoka nje ya kambi kiholela na kushiriki katika kufanya matukio ya kiharifu.
Waziri Mkuu ametangaza uamuzi huo leo (Jumanne, Februari 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa umma katika ya Halmashauri ya Kibondo.
”Vitendo vya uhalifu wilayani Kibondo vikiwemo vya utekaji wa watoto vimeongezeka na kusababisha hofu na taharuki miongoni mwa wananchi.”
Waziri Mkuu amesema ni vema halmashauri hiyo ikaandaa utaratibu wa kutoa vibali vitakavyowaruhusu Watanzania kupeleka bidhaa ndani ya kambi hivyo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wananchi waliopewa dhamana ya kufanya kazi kwenye kambi za wakimbizi wawe waadilifu na wasimamie sheria.
“Nafahamu tunao watendaji wetu ambao wapo kambini kusimamia shughuli mbalimbali za wakimbizi, tekelezeni wajibu wenu ipasavyo na si vinginevyo.”
Baada ya kuzungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Kibondo, Waziri Mkuu alikwenda wilayani Kakonko na kukagua mradi wa maji Muhange.
Pia Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya wilaya ya Kakonko unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 4.5.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 19, 2019.