Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba Aonya Wageni Wanaoanzisha Makampuni Kutumia Kivuli cha Wazawa.
Feb 16, 2026
Waziri Mkuu Mwigulu Nchemba Aonya Wageni Wanaoanzisha Makampuni Kutumia Kivuli cha Wazawa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba, akikaguan Mradi wa Bomba la Mafuta Chongoleani Mkoani Tanga.
Na Mwandishi Wetu - MAELEZO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amewatahadharisha wawekezaji na wageni wanaoanzisha makampuni kwa kutumia majina ya wazawa ili kunufaika na fursa za ‘Local Content’, akisema Serikali haitasita kuwafungia na kuwazuia kufanya kazi nchini watakaobainika kukiuka taratibu.

Dkt. Nchemba ametoa onyo hilo leo Februari 16, 2026 alipokagua mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima, Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, akieleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wake ambao umefikia asilimia 81.

Amesema mradi huo wa kimkakati wenye thamani ya dola za Marekani bilioni 5 ni  kielelezo cha undugu na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Uganda, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni.

“Ninatambua msisitizo uliowekwa na viongozi wetu katika utekelezaji wa mradi huu. Tutaendelea kuweka uzito unaostahili kwa heshima ya undugu wetu, lakini pia kwa kulinda uhuru wetu kama nchi inayoweza kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati,” amesema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali imebaini uwepo wa baadhi ya wageni wanaotumia majina ya Watanzania kuanzisha makampuni yanayodaiwa kuwa ya wazawa, ilhali umiliki wake si halali, kwa lengo la kujinufaisha na masharti ya ushirikishwaji wa Watanzania katika mradi huo.

“Tunataka kuinua kampuni za Watanzania. Wapo wasio waaminifu wanaotumia anuani za Watanzania ambao si wanufaika halisi. Watakaogundulika kufanya ujanja huo tutawafungia na hawatafanya kazi tena nchini,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa kufanya hivyo ni kuwatapeli na kuwaibia Watanzania fursa walizotengewa katika miradi mikubwa ya maendeleo. “Tumekupa mradi una nafasi yako, tunataka inufaike kwa Watanzania. Mkiwaibia wananchi fursa hizi, tutachukua hatua kali,” amesema Dkt. Nchemba.

Amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa masharti ya ‘Local Content’ ili kuhakikisha miradi mikubwa ya kimkakati inaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi na kuchochea uchumi wa ndani.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi