Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Samia Ateuliwa Kinara wa Afya ya Uzazi Mama na Mtoto Afrika.
Feb 16, 2026
Rais Samia Ateuliwa Kinara wa Afya ya Uzazi Mama na Mtoto Afrika.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ateuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.
Na Timothy Mwaikyenda - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameteuliwa kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika katika masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mheshimiwa Mahmoud Thabit Kombo amesema hayo leo Februari 16, 2026 wakati wa mkutano na waandishi wa habari, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Amesema uteuzi huo umefanywa na Mkutano Mkuu wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika, kwa kutambua juhudi za Rais Samia katika kupambana na kupunguza vifo vya mama na mtoto nchini.

Waziri Kombo amesema kupitia nafasi hiyo Rais Samia atakuwa na jukumu la kuhamasisha nchi wanachama kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kufanya tathmini za mara kwa mara kuhusu maendeleo ya sekta ya afya ya uzazi, mama na mtoto barani Afrika.

Amesema uteuzi huo unaifanya Tanzania kuendelea kuonesha dhamira ya kuchangia uongozi wa Bara la Afrika katika kujenga mifumo imara ya afya inayolinda haki ya kila mwanamke na mtoto kupata huduma bora.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, akizungumza wakati wa mkutano huo amesema Rais Samia alianza kuonesha dhamira thabiti ya kupunguza vifo vya mama na mtoto tangu mwaka 2016 alipokuwa Makamu wa Rais.

Ameeleza kuwa kupitia kampeni aliyoianzisha ya kuzuia vifo vya mama na mtoto, Tanzania imepiga hatua kubwa ambapo kiwango cha vifo vya uzazi kilipungua kutoka takribani vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

Dkt. Shekalaghe amesema mafanikio hayo yametokana na msisitizo na ufuatiliaji wa karibu wa ajenda hiyo, huku akibainisha kuwa uteuzi huo ni heshima kwa Taifa na chachu ya kuimarisha zaidi huduma za afya ya uzazi nchini na barani Afrika kwa ujumla.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi