Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesisitiza wakandarasi na wasimamizi wa miradi katika maeneo mbalimbali nchini kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili wananchi waanze kunufaika na miradi hiyo.
Pia amewasisitiza wahakikishe miradi yote inayotelelezwa inaedana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na ahadi ya siku 100 za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ametoa msisitizo huo leo Februari 13, 2025 wakati wa ukaguzi wa mradi wa Kituo cha kupoozea umeme jijini Tanga.

“Nitoe rai kwa wakandarasi; kazi iliyoko eneo la mradi lazima iendane na fedha walizokwisha kuzipokea. Kasi ya utekelezaji wa mradi iendane na fedha zinazotolewa na Serikali,” amesisitiza Waziri Mkuu.
Dkt. Nchemba amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini, akisisitiza kuwa utekelezaji huo unapaswa kuzingatia thamani ya fedha ili kurahisisha huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa mradi wa Kituo cha Kupoozea umeme umegharimu zaidi ya shilingi trilioni 1, ukiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama tawala.

Kwa upande wa utekelezaji wa ahadi za siku 100 za Mheshimiwa Rais, Waziri Mkuu amesema katika sekta ya elimu Serikali imeajiri walimu zaidi ya 7,000, huku sekta ya afya ikiajiri watumishi wapatao 5,000, akibainisha kuwa hatua hizo zimekamilika kabla ya kutimia kwa siku 100.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza ahadi katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya afya ambapo imeanzisha mfumo wa bima ya afya kwa wote unaojumuisha makundi maalum kama wakina mama, watoto na wazee.
Katika sekta ya viwanda, ameeleza kuwa Serikali imeendelea kuanzisha viwanda vipya na kuboresha vilivyopo ili kuongeza ajira na kukuza uchumi wa wananchi.

Aidha, Waziri Mkuu amewasihi wananchi kuzingatia sheria, taratibu na kuimarisha undugu na mshikamano akizitaka Kamati za Ulinzi na Usalama katika maeneo mbalimbali kusimamia kwa karibu migogoro kati ya wakulima na wafugaji kwa kuzingatia matumizi bora ya ardhi ili kudumisha amani na umoja wa kitaifa.