Dodoma. Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inatekeleza mradi wa ujenzi wa vyuo 64 vya ufundi stadi katika wilaya mbalimbali nchini pamoja na chuo kimoja katika Mkoa wa Songwe, mradi unaogharimu takribani shilingi bilioni 100.
Hayo yameelezwa leo Februari 16, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa VETA, CPA Anthony Kasore, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mtumba – Dodoma.

CPA Kasore amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha elimu ya ufundi stadi na kuongeza fursa za ajira kwa vijana nchini. “Ujenzi unaendelea katika wilaya 64 na kimoja katika Mkoa wa Songwe. Ujenzi huu unagharimu takribani shilingi bilioni 100,” amesema.
Amesema kwa sasa, VETA ina vyuo 80 vilivyosambaa kote nchini vinavyohudumia zaidi ya wanafunzi 86,000 kwa mwaka. Serikali inalenga kuhakikisha kila wilaya inakuwa na angalau chuo kimoja cha VETA ili kuongeza udahili.
CPA Kasore ameongeza kuwa matarajio ni VETA kuwa na jumla ya vyuo 152 ifikapo mwaka 2027 hatua itakayoongeza udahili hadi wanafunzi 250,000 kwa mwaka.

Sambamba na upanuzi wa miundombinu hiyo amesema Serikali kupitia VETA imehuisha mitaala na kubuni programu mahsusi zinazolenga kuwawezesha vijana, wanawake na makundi mbalimbali kupata ujuzi utakaowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.

Aidha, amesema katika mwaka huu wa masomo VETA imeboresha utaratibu wa udahili kwa kuondoa mtihani wa mchujo (aptitude test) ili kutoa fursa kwa waombaji wengi zaidi ambapo jumla ya waombaji 18,875 wamechaguliwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi mwaka huu, na hadi Februari 10, 2026 wanafunzi 7,952 walikuwa tayari wameripoti vyuoni.

Amesema hatua hizo zinatarajiwa kupanua wigo wa elimu ya ufundi stadi, kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira na kuongeza nguvu kazi yenye ujuzi stahiki kwa maendeleo ya Taifa.