WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inafanya jitihada kuhakikisha tatizo la usafiri kwa wananchi wa Mafia linakwisha.
"Nataka niwahakikishie wananchi wa Mafia kwamba kazi inaendelea vizuri na hivi karibuni watapata usafiri wa uhakika."
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi (Alhamisi, Agosti 13, 2020) kwenye karakana na meli ya Songoro iliyoko Kigamboni, Dar es Salaam mara baada ya kukagua ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia ambacho kitafanya kazi kati ya Mafia na Nyamisati mkoani Pwani.
Amesema hivi sasa wananchi wa Mafia wanapata usafiri kwa kivuko ambacho kinatoa huduma mara tatu kwa wiki kilichotolewa Zanzibar. "Hicho kitaendelea kutoa huduma hadi hiki kikamilike na kiende huko", amesisitiza.
"Nimekuja kuangalia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kivuko kwani dhamira ya Serikali yetu ni kuhakikisha usafirishaji nchini unaimarishwa kwenye maeneo yote ukiwemo wa majini."
Akizungumzia suala la ajira, Waziri Mkuu amesema anapata faraja sana kuwaona Watanzania wakichapa kazi kwa bidii. "Napata faraja sababu Serikali imejitajidi kupambana na changamoto ya ajira, na ajira siyo lazima iwe ya kukaa ofisini. Hapa nimewaona wazawa wakifanya kazi, kuanzia mmiliki hadi mafundi.”
“Ninyi ni mabalozi wa ajira kwa Watanzania sababu yako mataifa yalidai kuwa Watanzania hawaajiriki kwani siyo waadilifu, ni wadokozi. Lakini hapa sijasikia Mkurugenzi wa Songoro Marine akisema kuwa mmedokoa spana au nyaya. Ninyi ni uthibitisho kuwa Watanzania tunaajirika, ninawapongeza sana," amesema Waziri Mkuu na kushangiliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameliagiza Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania(TASAC) lihakikishe kuwa linafanya kazi karibu na kampuni ya Songoro ili liweze kufuatilia ujenzi wa kivuko hicho na kutoa kibali cha kuendelea na kazi nyingine kila inapohitajika kufanya hivyo.
"Haifai mtu afanye kazi hadi amalize halafu anakuomba cheti cha kuthibitisha ubora wake, wewe ndiyo unakuja kutoa kasoro. Ni vema mfanye kazi kwa karibu, waiteni wakague kila hatua ili mkimaliza tu, wanakuwa wanajua nini kimefanyika," amesisitiza.
Mapema, akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kivuko hicho, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Mhandisi Japhet Maselle alisema kivuko hicho ambacho ujenzi wake umefikia asilimia 83, kinatarajiwa kukamilika ifikapo Septemba 25, mwaka huu.
Alisema licha ya kutatua kero ya usafiri kwa abiria, kukamilika kwa ujenzi wa kivuko kipya cha Mafia, kutatoa fursa za kibiashara kwa wakazi wa Mafia.
Alisema ujenzi wa kivuko hicho utagharimu sh. bilioni 5.2 huku mkandarasi akiwa ameshalipwa sh. bilioni 4.2 sawa na asilimia 80 ya gharama yote.
"Kivuko hiki kipya chenye urefu wa mita 42 na upana wa mita 12, kitakapokamilika kitakuwa na uwezo wa kubeba tani 100 yaani abiria 200, magari madogo 10 na mizigo."
Waziri Mkuu ameendelea na ziara yake ya kufuatilia maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli aliyoyatoa wiki iliyopita akiwa njiani kurejea Dar es Salaam.