Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dar es salaam
Waziri wa Kilimo Mhe Prof. Adolf Mkenda leo Septemba 2, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkazi wa Kampuni ya Wilmar Tanzania, Sachin Suman katika ofisi za Wizara ya Kilimo zilizopo katika eneo la Tazara Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkenda amekutana na Mkurugenzi huyo ambapo Kampuni yake inamiliki viwanda vikubwa 3 mkoani Morogoro na kuwahakikishia kuwa atatekeleza maagizo yaliyotolewa na Serikali kwa viongozi wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Uwekezaji na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuondoa urasimu unaokwamisha ujenzi wa viwanda nchini.
Katika mkutano huo Waziri Mkenda amesema kuwa wamekubaliana kuhusu kuongeza uwekezaji katika ukoboaji wa mpunga ili kuhakikisha kwamba unapatikana mchele mzuri ambao utakuwa unauzwa zaidi kimataifa.
Amesema kwa sasa kiwanda hicho kina uwezo wa kukoboa tani 100,000 kwa mwaka za mpunga jambo ambalo amekitaka kiwanda hicho kuongeza uwezo wake kwani wana uwezo wa kufikia mpaka tani 300,000 kwa mwaka kwa kuanzia.
Waziri Mkenda ameeleza kuwa kwa kauli moja mkutano huo umekubaliana kuunda timu ya wataalamu kutoka serikalini pamoja na kampuni hiyo ili ndani ya siku 30 itatakiwa kuangalia maeneo mazuri ya kulima mpunga na kutoa mapendekezo ya namna kilimo hicho kitakavyofanyika ili kuongeza tija na uzalishaji.
Amesema kuwa kiwanda cha kukoboa mpunga (Murzar Wilmar Rice Mills Ltd) kilichojengwa kwa gharama ya shilingi Bilioni 48 na ambacho kina uwezo wa kukoboa tani 288 za mpunga kwa siku na kisha kufungasha mchele katika ujazo na madaraja mbalimbali kitatoa fursa kwa wakulima kujihakikishia soko la uhakika wa mpunga.
Kiwanda hicho kimeajiri wafanyakazi 75 na kinanunua mpunga kutoka kwa wakulima takribani 5,000 kutoka Mikoa ya Morogoro, Mbeya, Shinyanga na Tabora ambapo katika mwaka 2020 kimenunua tani 65,000 zenye thamani ya shilingi Bilioni 45.
Waziri Mkenda amesema kuwa miongoni mwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo ni pamoja na kuwa na mashamba darasa kwa ajili ya wakulima na kuwa na maeneo ya kukusanyia mazao ya kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kupeleka viwandani.
Waziri Mkenda amesema kuwa S+erikali italifanyia kazi kwa haraka ombi lao la kupatiwa kibali na serikali kuzalisha umeme utakaotumika katika shughuli za kiwanda na mwingine utakaosalia wataliuzia Shirika la Umeme (TANESCO).
Kuhusu uzalishaji wa mazao ya mafuta ikiwemo alizeti na Soya kwa ajili ya kuzalisha mafuta mengi ya kula, Waziri Mkenda amesema kuwa kampuni hiyo ipo tayari kununua mazao hayo na kuyachakata, hivyo amewahakikishia kuwa serikali ina mkakati madhubuti wa kuhakikisha uzalishaji wa alizeti unaongezeka kwa kiasi kikubwa ikiwemo uzalishaji wa michikichi.
Mhe Prof. Mkenda ameipongeza kampuni ya Murzar Wilmar Rice Mills Ltd kwa kuwekeza katika kiwanda hicho kikubwa kuliko vyote hapa nchini kwa kukoboa mpunga.